1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vifo vya wahamiaji wanaovuka bahari kwenda Ulaya vyazidi

14 Julai 2021

Shirika la UN linaloshughulikia Uhamiaji, IOM limesema idadi ya wahamiaji na wakimbizi waliokufa wakati wakijaribu kufika barani Ulaya kupitia safari za hatari kwenye bahari ya Mediterania imeongezeka maradufu

Libyen I Flüchtlinge im Mittelmeer
Picha: Sergi Camara/AP/dpa/picture alliance

Ripoti hiyo imesema watu wapatao 1,146 walikufa na kwamba idadi ya vifo iliongezeka kwa asilimia 58 katika kipindi hicho. Shirika hilo la IOM limesema kuwa njia ya Kati ya bahari hiyo ya Mediterenia kati ya Libya na Italia ilikuwa mbaya zaidi ambapo watu 741 walifariki. Njia nyingine mbaya ilikuwa ile inayotokea bahari ya Atlantiki kati ya Afrika Magharibi na visiwa vya canary nchini Uhispania ambapo watu 250 walipoteza maisha.

Kiasi cha watu 149 pia walifariki dunia katika njia ya Magharibi mwa Mediterenia kuelekea Uhispania pamoja na wengine sita katikaeneo la Mashariki mwa Mediterenia kuelekea Ugiriki. Shirika hilo la IOM linasema kuwa idadi kamili ya vifo katika njia za bahari kuelekea Ulaya huenda ikawa juu zaidi kwasababu meli nyingi zilizozama haziripotiwi na nyingine huwa vigumu kuthibitisha .

Mashirika ya msaada wa kibinadamu yatoa onyo

Mashirika  ya misaada ya kibinadamu yameonya kuwa ukosefu wa vifaa vya serikali vya uokoaji na utafutaji hasa katika eneo la Kati mwa Mediterenia huenda ukafanya hatua ya wahamiaji kuvuka bahari hiyo kuwa hatari zaidi huku mataifa ya bara Ulaya yakiongeza utegemeaji wa msaada kutoka kwa mataifa ya Kaskazini mwa Afrika  yenye raslimali chache za kushughulikia operesheni za utafutaji na uokoaji.

Meli ya uokoaji ya Geo Barents katika bahari ya MeditereniaPicha: Avra Fialas/MSF/Handout via REUTERS

Ripoti hiyo imeendelea kusema kuwa Tunisia iliongeza operesheni kama hizo kwa asilimia 90 katika miezi sita ya kwanza ya mwaka huu wa 2021 huku mamlaka nchini Libya ikiwanasa na kuwarejesha nyumbani zaidi ya wanaume elfu 15, wanawake na watoto hii ikiwa ni idadi mara tatu zaidi ya watu katika kipindi sawa na hicho mwaka jana .

Serikali ya Italia yazilenga meli za mashirika yasiokuwa ya kiserikali

Wakati huo huo, serikali nchini Italia iliendelea kuzilenga meli za uokoaji ambazo zimeshughulika kwa miaka mingi kujaza pengo lililoachwa na serikali za Ulaya, huku ikizuia mara kwa mara meli zinazoendeshwa na mashirikia yasiokuwa ya kiserikali kwa miezi na wakati mwingine miaka kadhaa. Msemaji wa shirika hilo la IOM Safa Msehli , amesema kuwa licha ya masuala mengi kuchangia katika ongezeko la idadi hiyo mwaka huu yanayojumuisha ongezeko la maboti hafifu yanayojaribu kuvuka bahari, ukosefu wa operesheni thabiti za utafutaji na uokoaji za serikali zinazoongozwa na bara Ulaya katika bahari hiyo ya kimataifa pamoja na vikwazo dhidi ya mashirika hayo yasiokuwa ya kiserikali yalikuwa miongoni mwa masuala makuu.

Katika miaka ya hivi karibuni, makundi ya kutetea haki za binadamu yameripoti kuhusu mateso na ukiukaji wa haki za wahamiaji na wakimbizi kutoka kwa walinzi wa Pwani ya Libya baada ya kunaswa na kuzuiwa katika vituo vya vizuizi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW