UN: Vikosi vya Afghanistan, washirika wameua raia zaidi 2019
30 Julai 2019Ripoti hiyo iliyotolewa leo inazungumzia raia waliouawa wakati wa ooeresheni za kijeshi za Marekani dhidi ya waasi, kama vile mashambulizi ya ndege na operesheni za usiku dhidi ya maficho ya wapiganaji.
Takwimu hizo za karibuni kuhusu wahanga wa vita vya Afghanistan zimetolewa wakati ambapo mazungumzo kati ya kundi la Taliban namaafisa wa Marekani kumaliza vita vya miaka 18 nchini Aghanistan yameingia hatua muhimu, ambapo wajumbe wa majadiliano wa Marekani wanalenga kufikia makubaliano ya amani kabla ya Septemba 1.
Marekani ilihitimisha rasmi ujumbe wake wa mapambano nchini Afghanistan mnamo mwaka 2014 lakini bado inaendelea kutoa msaada wa angani na mwingine kwa vikosi vya Afghanistan vinavyopambana na makundi ya wapiganaji.
Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema raia 403 waliuawa na vikosi vya Afghanistan katika miezi sita ya kwanza ya mwaka huu na wengine 314 waliuawa na vikosi vya kimataifa na kufanya jumla ya watu 717.
Hiyo inalinganishwa na watu 531 waliouawa na wapiganaji wa kundi la Taliban, kundi lenye mafungano na Dola la Kiislam na wapiganaji wengine katika kipindi sawa.
Imesema 300 kati ya waliouawa na wapiganaji walilengwa moja kwa moja. Kundi la Talibana limekuwa likiendesha mashambulizi ya karibu kila siku, yakilenga hasa vikosi vya usalama.
Hakukuwa na tamko la mara moja kutoka kwa serikali mjini Kabul au jeshi la Afghanistan kuhusu ripoti hii.
Lakini afisa wa NATO amesisitiza kuwa muungano huo haujihusishi na mapambano nchini Afghanistan, bali unatoa mafunzo, ushauri na msaada kwa vikosi vya usalama vya nchi hiyo.
Trump ataka kupunguza wanajeshi ifikapo uchaguzi wa 2020
Ripoti imetolewa huku waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo, akifahamisha kuwa Rais Donald Trump amemuagiza kupunguza vikosi vya mapambano vya Marekani nchini Afghanistan kufikia uchaguzi mkuu wa mwakani.
"Hilo ndiyo agizo langu kutoka kwa rais wa Marekani. Amekuwa muwazi zaidi - maliza vita visivyoisha. Punguza. Hatutokuwa sisi peke yetu. Tunatumai kwamba kwa ujumla haja ya kuwepo na vikosi vya mapambano katika kanda hiyo imepungua," alisema Pompeo katika mazungumzo na klabu ya wanauchumi.
Kutangazwa kwa ratiba hiyo kutaongeza uvumizi kwamba Trump amejiandaa kufikia makubaliano yoyote na Taliban ambayo yataruhusu angalau kuondolewa kwa sehemu wanajeshi wake kabla ya uchaguzi, bila kujali wasiwasi wa serikali ya mjini Kabul inayoungwa mkono na Marekani.
Matamshi ya Pompeo pia yamekuja wakati mgumu, ambapo Marekani inajiandaa kwa duru nyingine ya mazungumzo na waasi. Kutangaza malengo ya Trump kuhusu kupunguza vikosi huenda kukadhoofisha nafasi ya majadiliano ya Marekani iwapo Wataliban wataamini Trump anataka kutekeleza uondaoji huo, bila kujali maelezo muhimu ya makubaliano hayo.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre, ape,rtrtv
Mhariri: Josephat Charo