1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Vita vya magenge Haiti sasa ni 'janga' katika mashamba

29 Novemba 2023

Vita vya magenge ya uhalifu nchini Haiti vimeenea kutoka mji mkuu hadi maeneo muhimu ya mashambani, na kuwafanya maelfu ya watu kuyakimbia makazi yao na pia kusababisha athari mbaya katika upatikanaji wa vyakula muhimu

Kiongozi wa muungano wa G9 nchini haiti Jimmy ''Barbacue'' Cherizier, (katikati) aongoza maandamano dhidi ya waziri mkuu wa nchi hiyo Ariel Henry mjini Port -au-Prince mnamo Septemba 19, 2023
Kiongozi wa muungano wa G9 nchini haiti Jimmy ''Barbacue'' Cherizier, (katikati) aongoza maandamano dhidi ya waziri mkuu wa nchi hiyo Ariel HenryPicha: Ralph Tedy Erol/REUTERS

Vurugu zimeongezeka kwa hatua katika eneo la Bas-Artibonite lililoko kaskazini mwa mji mkuu Port -au- Prince, ambalo linazalisha kwa wingi vyakula muhimu kama vile mchele, huku Umoja wa Mataifa ukisema kuwa takribani watu 22,000 wamepoteza makazi yao wakati mauaji yakiendelezwa, uporaji, utekaji nyara na ukatili mkubwa wa kijinsia.

Ripoti hiyo imefichua kuwa magenge ya uhalifu yenye nguvu zaidi katika eneo hilo yanahusishwa na wanachama wa muungano wenye nguvu wa G-Pep katika mji huo mkuu, na kusema hii inaonesha mkakati wa muungano huo wa G-Pep wa kuimarisha ushawishi wake.

Soma pia:Jeshi la polisi nchini Haiti limeelemewa na wingi wa magenge na uhalifu unaofanywa na magenge hayo

Ripoti hiyo imeongeza kuwa wakiwa wamejihami kwa bunduki na bastola, magenge hayo yamechoma nyumba, kushambulia mifumo ya umwagiliaji maji mashamba, kuiba mazao na mifugo na kudai kodi kutoka kwa wakulima kuwawezesha kufikia mashamba yao.

Msaada wa kibinadamu wapungua

Vurugu hizo zimepunguza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa msaada wa kibinadamu katika eneo hilo, na kuachia jukumu hilo la msaada kwa waathiriwa wa ukatili wa kijinsia kwa vyama vya kijijini vyenye uhaba wa fedha.

Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa - Volker TurkPicha: KHALED DESOUKI/AFP

Ripoti hiyo imeongeza kuwa ni nadra kwa waathiriwa kujitokeza kutokana na hofu ya mashambulizi ya kisasi na hali ya kutowaamini maafisa wa polisi.

Soma pia:Mahakama Kenya yaongeza amri ya kuzuia polisi kupelekwa Haiti

Ukosefu wa usalama na kupungua kwa fedha kumesababisha makundi ya msaada kusitisha shughuli zao na kupunguza bajeti huku Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa likikadiria kuwa takriban nusu ya idadi ya watu nchini humo inakabiliwa na njaa, ikiwa ni pamoja na zaidi ya asilimia 45 ya watu katika eneo la Bas-Artibonite.

Volker Turk atoa wito wa kupelekwa haraka  kwa vikosi vya kimataifa nchini Haiti

Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk, amesema ombi la msaada wa maafisa wa usalama lililotolewa na serikali ya Haiti na kuidhinishwa na Umoja wa Mataifa mwezi uliopita, linapaswa kutekelezwa mara moja.

Soma pia:Bunge la Kenya yaidhinisha polisi kutumwa nchini Haiti

Turk amesema hali hiyo imekuwa janga na akasisitiza wito wa kuletwa kwa vikosi hivyo vya kimataifa na kuchukuliwa kwa hatua zaidi za serikali, vikwazo zaidi na udhibiti mkubwa wa silaha zinazoaminika kuingizwa nchini humo kwa kiasi kikubwa kutoka Marekani.

Kikosi kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, na kuongozwa na Kenya kimeidhinishwa, lakini huenda kikachukuwa miezi kadhaa kabla ya kupelekwa nchini humo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW