UN: vitendo vya RSF el-Fasher vyaashiria mauaji ya halaiki
20 Februari 2026
Taarifa iliyotolewa jana na ujumbe huru uliopewa jukumu la kutafuta ukweli katika mzozo wa Sudan, umesema kuwa wanamgambo wa RSF walifanya mauaji ya halaiki na ukatili mwingine katika mji wa el-Fasher baada ya kuuzingira kwa miezi 18 ambapo waliweka masharti "yaliyokusudiwa kusababisha maafa makubwa" kwa jamii zisizo za Kiarabu, hasa zile za Zaghawa na Fur.
Maafisa hao wa Umoja wa Mataifa wamesema maelfu ya raia waliuawa wakati RSF ilipochukua udhibiti wa mji wa El-Fasher, ngome pekee iliyokuwa imesalia mikononi mwa jeshi la Sudan huko Darfur.
Wajumbe hao wameendelea kueleza kuwa ni asilimia 40 pekee ya wakazi 260,000 wa jiji hilo ndio walionusurika na kufanikiwa kukimbia huku maelfu miongoni mwao wakijeruhiwa na hatima ya wengine ikiwa hadi sasa bado haijulikani.
Wajumbe hao wa kuusaka ukweli wamesema angalau vigezo vitatu vinavyozingatiwa ili uhalifu kuwa mauaji ya kimbari vilishuhudiwa huko El-Fasher ikiwa ni pamoja na muundo wa kimfumo wa mauaji ya kikabila, unyanyasaji wa kingono, uharibifu na matamshi ya wazi yanayohimiza waziwazi kuangamizwa kwa jamii zisizo za Kiarabu.
Vitendo vya RSF vilipangwa
Mwenyekiti wa Ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa wa Kutafuta Ukweli katika vita vya Sudan, Mohamed Chande Othman ambaye aliwahi pia kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania amesema uhalifu uliofanywa na RSF ulipangwa na una viashiria vya mauaji ya halaiki akisisitiza kuwa RSF waliuzingira mji, wakazuia upatikanaji wa chakula, maji, umeme na vifaa vya matibabu huku wakishambulia kwa droni maeneo ya makazi, kambi za wakimbizi, masoko na maeneo ya ibada.
" Athari za muda mrefu za yote hayo, zilipelekea hali kuwa ngumu zaidi kwa jamii zilizoathiriwa, huku watu hao wakiishi maisha yasiyofaa kwa binaadamu."
Kulingana na Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, waasi wa RSF walivamia el-Fasher mwezi Oktoba mwaka jana na kuushambulia mji huo kwa nguvu kubwa iliyojaa ukatili ikiwa ni pamoja na mauaji ya halaiki, unyanyasaji wa kingono, mateso na utekaji nyara. Kati ya Oktoba 25 na Oktoba 27 watu 6,000 waliuawa , huku ghasia za RSF katika kambi ya wakimbizi ya Abu Shouk, nje kidogo ya el-Fasher, zikisababisha mauaji ya watu wasiopungua 300 katika muda wa siku mbili.
Waasi wa RSF hawakujibu barua waliotumiwa na shirika la habari la AP likiwataka kutoa maoni yao kuhusu ripoti hii, lakini kiongozi mkuu wa kundi hilo, Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo, amewahi kukiri vitendo vya unyanyasaji vilivyofanywa na wapiganaji wake, lakini akapinga ukubwa unaotajwa wa ukatili huo. Jana Alhamisi, Marekani iliwawekea vikwazo makamanda watatu wa RSF kutokana na vitendo vyao huko el-Fasher, na kulitaka kundi hilo kuchukua hatua za kusitisha mapigano mara moja.