1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Watetezi wa amani wanawake wana hali mbaya kiusalama

Angela Mdungu
19 Januari 2022

Wanawake wanaotafuta kuchagiza, kudumisha amani na kulinda haki za binaadamu wanakabiliwa na hali mbaya hivi sasa zaidi ya ilivyokuwa kabla ya janga la virusi vya corona

Schweiz Genf | UN-Hochkommissarin für Menschenrechte zu Äthiopien, Tigray
Picha: Denis Balibouse/REUTERS

Hayo yamesemwa na kamishna mkuu wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa Michelle Bachellet alipokuwa akizungumza katika baraza la usalama la umoja wa mataifa Jumanne 18.01.2022. 

Bachelet alisema kwa mwaka 2020, ofisi yake ilithibitisha mauaji ya wanawake 35 watetezi wa haki za binadamu, waandishi wa habari na wanachama wa vyama vya wafanyakazi. Mauaji hayo yamerekodiwa kutoka kwenye mataifa saba yenye mizozo ambayo yanatoa takwimu. Amesema, idadi hiyo ambayo kwa hakika ni ndogo kuliko uhalisia ilipita ile ya mauaji ya mwaka 2018 na 2019 yaliyothibitishwa.

Akizungumza katika mjadala wa wazi  wa baraza la usalama kuhusu wanawake, amani na usalama Bachelet amebainisha kuwa, maamuzi yanayohusu amani yasiyoakisi sauti za wanawake, uhalisia na haki, siyo endelevu. Amesisitiza kwamba ni lazima kuwe na utetezi wa wazi kwa ajili ya uwekezaji sahihi kwa watetezi wa haki za wanawake na wanaotafuta kudumisha amani –kwa kuondoa vikwazo kama vile pengo la kidijitali: kuongeza ufadhili wa kifedha na kuongeza kwa kiasi kikubwa uwajibikaji dhidi ya mashambulizi na vitisho.

Mkuu huyo wa haki za binadamu wa umoja wa mataifa ameongeza kuwa, ofisi yake iliyo mjini Geneva ilirekodi visa vya mashambulizi dhidi ya wanawake wanaojishughulisha na masuala ya haki ya usawa wa kijinsia, afya ya uzazi, rushwa, haki za wafanyakazi bila kusahau masuala ya ardhi na mazingira

Licha ya azimio la baraza la usalama la umoja wa mataifa la mwaka 2000 la ushiriki sawa wa wanawake katika majadiliano ya kutafuta amani, Bachelet amesema, kati ya mwaka 1992 na 2019  asilimia 13 ya wasuluhishi wa amani,  asilimia 6 ya wapatanishi na watia saini wa michakato mikubwa ya amani duniani kote pekee walikuwa wanawake.

Maeneo yenye mizozo yameathiriwa zaidi

Hiyo ilikuwa kabla ya kuzuka kwa janga la virusi vya corona mwanzoni mwa mwaka 2020 na kabla ya wimbi la mizozo inayoendelea kutokota, mabadiliko ya  kisiasa yasiyo ya demokrasia na migogoro ya kiutu iliyoshuhudiwa katika jamii nyingi.

Maandamano ya wanawake kupinga kuminywa kwa haki zao AfghanistanPicha: ALI KHARA/REUTERS

Alitolea mifano ya hali ilivyo katika maeneo matatu ya mizozo  zikiwemo Afghanistan, Myanmar na ukanda wa Sahel huku akiliasa baraza la usalama la umoja wa mataifa kuwawajibisha wanaokiuka haki za binadamu zikiwemo za wanawake

Kwa upande wa ukanda wa Sahel, kamishna mkuu wa haki za binadamu wa umoja wa mataifa amesema ukosefu wa uwezeshwaji wa wanawake ni sababu kuu ya wazi katika mzozo wa kimaendeleo, kiusalama na kiutu kwenye eneo hilo. Akizungumzia Myanmar ameeleza kuwa watetezi wa haki za binadamu wanawake, walikuwa muhimu katika kudumisha amani lakini tangu jeshi lilipoingia madarakani mnamo Februari mwaka 2020, mashirika mengi ya kiraia yamelazimika kufungwa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW