1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watotot 10,000 wauawa, kujeruhiwa kwenye migogoro duniani

Sylvia Mwehozi
28 Juni 2018

Ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa inaonesha kuwa zaidi ya watoto 10,000 waliuawa au kulemazwa katika vita na migogoro uniani kote mwaka jana, wakati mwingine wakibakwa, kulazimika kutumikishwa kama wapiganaji.

Südsudan - Kindersoldaten
Picha: Getty Images/AFP/C. Lomodong

Kwa mujibu wa ripoti ya kila mwaka ya Umoja wa Mataifa kuhusu watoto na migogoro ya silaha, Jumla ya visa 21,000 vya ukiukaji wa haki za watoto vimeripotiwa mwaka 2017, ikiwa ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na visa vilivyoripotiwa mwaka 2016.

Umoja wa Mataifa unashutumu muungano wa kijeshi wa kiarabu unaoungwa mkono na Marekani katika mapigano ya Yemen, kwa kusababisha angalau nusu ya zaidi ya vifo 1,300 au majeruhi yaliyoripotiwa katika taifa hilo maskini.

Watoto walikuwa ni waathirika wa mashambulizi ya anga na ardhini yaliyofanywa na Saudia Arabia sambamba na Umoja wa Falme za Kiarabu yakiwalenga waasi wa Kihouthi wanaoipinga serikali ya Yemen inayotambulika kimataifa.

Idadi ya watoto wanaoajiriwa kama wanajeshi yapungua

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa Virginia GambaPicha: imago/Xinhua

Miongoni mwa madhila yaliyo orodheshwa katika ripoti hiyo ni askari watoto wa umri mdogo wa miaka 11 waliopigana katika vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Yemen na katika mataifa mengine. Virginia Gamba ni mwakilishi maalumu wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto na migogoro ya silaha. "Tumethibitisha zaidi ya visa 8,000 vya kuwaajiri na kuwatumia watoto, zaidi ya kesi 10,000 za mauaji na majeruhi, zaidi ya kesi 900 za ubakaji na vitendo vingine vya ukatili wa jinsia, zaidi ya kesi 1,100 za mashambulizi katika shule na hospitali, zaidi ya kesi 2,500 za kutekwa na karibu kesi 1,400 za kunyimwa upatikanaji wa misaada ya kibinadamu."

Mwakilishi huyo anasema ripoti hiyo imemwacha katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akishikwa na mshangao. Visa elfu 21 vya ukiukaji wa haki za watoto vilijumuisha watoto 10,000 waliouawa au kujeruhiwa hususan katika nchi za Iraq, Myanmar, Jamhuri ya Afrika ya Kati, jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Sudan Kusini na Yemen.

Watoto wanaotumikishwa kama wanajeshi huko YemenPicha: Getty Images/AFP/S. Al-Obeidi

Kiasi hicho ni ongezeko la kutoka visa 15,000 vilivyoripotiwa mwaka 2016. Zaidi mwaklishi huyo anasema, "mwaka 2017 zaidi ya watoto 10,000 waliachiwa kutoka makundi yenye silaha ukilinganisha na wale 8000 walioajiriwa. Ikiwa kila mwaka tutafanikiwa kupunguza idadi ya wanaoajiriwa na kuongeza idadi ya wanaoachiwa mara mbili, tutapunguza idadi ya watoto wanaojikuta katika hali hii."

Watoto kuhusishwa na makundi ya itikadi kali

Kwa mujibu wa ripoti hiyo nusu ya watoto 881 waliothibitishwa kujeruhiwa nchini Nigeria ni kwasababu ya mashambulizi ya kujitoa muhanga ikiwemo kuwatumia watoto kama waripuaji. Zaidi ya watoto 1,900 walikamatwa kwasababu ya wazazi wao au wenyewe kuhusishwa na kundi la wanamgambo la Boko Haram.

Angalau watoto 1,036 waliwekwa kizuizini nchini Iraq kwa makosa yanayohusiana na usalama wa taifa, zaidi wakihusishwa na kundi linalojiita Dola la kiislamu IS. Kiasi ya watoto 1,221 waliajiriwa na kutumiwa kama wanajeshi huko Sudan Kusini. Kundi la Al-Shabab la nchini Somalia lilidaiwa kuwateka zaidi ya watoto 1,600, baadhi yake wakitumiwa na majeshi na wengine kuwa waathirika wa ukatili wa kijinsia.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP

Mhariri: Caro Robi

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW