1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Watoto 620,000 wanaougua ukimwi Afrika hawapokei dawa

10 Agosti 2021

Ripoti moja ya Umoja wa Mataifa inasema watoto katika bara la Afrika wanatelekezwa linapokuja suala la matibabu yanayohusiana na virusi vya ukimwi VVU.

AIDS-Aufklärungskampagnen zum Welt-AIDS-Tag
Picha: Saikat Paul/Pacific Press/picture alliance

Ripoti moja ya Umoja wa Mataifa inasema watoto katika bara la Afrika wanatelekezwa linapokuja suala la matibabu yanayohusiana na virusi vya ukimwi VVU. Ripoti hiyo inasema idadi kubwa ya watoto hao watafariki kabla kutimiza umri wa miaka miwili.

Shirika Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Ukimwi, UNAIDS, pamoja na washirika wake linaonya kwamba hatua zilizopigwa katika kuumaliza ugonjwa wa ukimwi miongoni mwa watoto wa hadi umri wa miaka 14, vijana na kina mama walio na umri mdogo, zimekwama kwa sasa, likisema halikutimiza hata moja ya malengo yake ya mwaka 2020. Kwa mara ya kwanza idadi ya watoto walio kwenye matibabu ya ugonjwa huo ilipungua.

Soma zaidi: Maambukizi ya HIV yaongezeka Ulaya mashariki na Asia ya Kati

Kulingana na ripoti hiyo, inakadiriwa kwamba watoto 620,000 wanaoishi na virusi vya ukimwi katika nchi 21 za Afrika walikuwa hawapokei dawa za kupunguza makali virusi vya HIV. Ni nchi sita tu kati ya ishirini na moja zilizotoa madawa hayo kwa watoto katika mwaka 2020. Nchi hizo ni Kenya, Eswatini, Lesotho, Malawi, Namibia na Zimbabwe.

Mkurugenzi wa idara ya mikakati ya shirika la UNAIDS Peter Ghys, anasema mapungufu yaliyoko katika kuwatibu watoto ugonjwa huu duniani ni changamoto kubwa. Takwimu zinaonyesha kwamba watu wazima ndio wanaopata matibabu zaidi ya watoto.

Ghys anasema kupungua kwa idadi ya watoto wanaopewa matibabu pia kumetokana na janga la virusi vya corona. Anasema mifumo ya matibabu ni tofauti katika nchi mbali mbali na nchi zengine zilikuwa zimejihami vyema. Nchi zilizo na mifumo duni ya matibabu zimeonekana kuwatelekeza watoto katika masuala ya matibabu ya virusi hivyo.

Mojawapo ya nchi zilizopambana vyema na matibabu ya watoto walio na ugonjwa huo ni Eswatini ambayo mkurugenzi huyo wa UNAIDS anasema licha ya kuwa ni nchi ndogo lakini ina uwezo wa kuwatibu watoto na hata watu wake wazima. Kwa upande mwengine, nchi zilizo na uwezo mdogo wa kimatibabu ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Angola, Chad na Burundi. Ghys anasema katika nchi hizo, kumekuwa na mchanganyiko wa sababu zilizosababisha matibabu miongoni mwa watoto yasitolewe ikiwemo, mifumo duni ya afya pamoja na masuala ya kisiasa kupewa kipau mbele.

Picha: Imago/F. Stark

Katika mahojiano na DW Ghys pia amesema kwamba imekuwa wazi kuwa katika miaka ya hivi karibuni, watoto wamekuwa hawapimwi virusi vya ukimwi wanapozaliwa au wanapimwa ila kuna mapungufu katika mifumo na watoto hao hata wanapopatikana na maambukizi, hawaanzishiwi matibabu. Ghys anasema ili kukabiliana na hali hii, hivi karibuni kumekuwa na mikakati mingine ya upimaji.

Soma zaidi: WHO yatoa muongozo wa kujipima mwenyewe HIV

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa inazidi kueleza kuwa, thuluthi mbili ya maambukizi miongoni mwa watoto mwaka 2020 yalikuwa katika nchi sita ambazo ni Nigeria, Msumbiji, Afrika Kusini, Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Zambia huku Nigeria ikiwa na idadi kubwa zaidi ambapo kati ya watoto watano, mmoja alikuwa ameambukizwa virusi hivyo.

Katika mahojiano na DW, Thembisile Xulu  ambaye ni mkurugenzi wa Baraza la Kitaifa la Ukimwi Afrika Kusini SANAC amesema nchini humo, unyanyapaa bado ni tatizo kubwa na kizingiti katika juhudi za kupambana na HIV.

Xulu ameongeza kwamba Afrika Kusini kwa sasa inashughulikia njia kadhaa za kuhakikisha kwamba malengo ya matibabu yanafikiwa. Anasema njia bunifu zinahitajika kuhakikisha kwamba watoto wadogo na vijana wanaendeelea na mipango yao ya matibabu.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW