Watu 1,260 wakamatwa Venezuela kufuatia vurugu za uchaguzi
13 Agosti 2024Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limeripoti kuwa karibu watu 1,300 wakiwemo watoto 100 wamekamatwa nchini Venezuela huku watu 23 wakifariki kufuatia vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi.
Baraza hilo limeelezea kwamba watu walikuwa wanakamatwa kiholela na wazazi hawajakubaliwa kuambatana na watoto wao kuelekea mahakamani.
Umoja wa Mataifa unasema kati ya 23 waliofariki kutokana na machafuko hayo ya uchaguzi, 18 walikuwa vijana chini ya umri wa miaka 30, wengi wao wakiuwawa kwa kupigwa risasi. Takwimu hizo zilichukuliwa kati ya Julai 28 na Agosti 8. Rais Nicolas Maduro, ambaye amekuwa mamlakani tangu mwaka 2013, alitangazwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika mwezi uliopita na tume ya uchaguzi nchini humo, ambayo inadaiwa kumuunga mkono.