1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Watu 13,000 waliuawa DRC mnamo miezi minane iliyopita

Daniel Gakuba
5 Juni 2020

Umoja wa Mataifa umesema kuwa watu 1,300 wameuawa katika muda wa miezi 8 iliyopita Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na wapatao nusu milioni wamelazimika kuzihama nyumba zao kutokana na ghasia.

Kongo | Flüchtlinge in Ituri
Picha: imago-images/Xinhua/A. Uyakani

Akiiwasilisha ripoti hiyo mjini Geneva mapema leo, Afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na haki za binadamu, Michelle Bachelet ameonya kwamba baadhi ya mauaji yaliyotokea na mashambulizi yaliyowalazimisha watu kuyapa kisogo makaazi yao, yanaweza kuchukuliwa kuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita.

Ofisi yake imesema idadi ya wahanga imeongezeka sana mnamo wiki za hivi karibuni, katika mizozo inayojiri kwenye mikoa mitatu ya mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, ambayo ni Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, ambayo imeacha athari mbaya sana kwa raia.

Michelle Bachelet, Mkuu wa Ofisi ya Umoja w Mataifa kuhusu Haki za BinadamuPicha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema makundi yenye silaha yamefanya mauaji ya halaiki, na pia vikosi vya serikali vimehusika katika uhalifu.

Vyombo ya serikali wahusishwa na uhalifu

Bi Bachelet amesema amechukizwa sana na ukatili unaokithiri dhidi ya raia, unaofanywa na makundi yenye silaha, huku pia vyombo vya usalama vya kitaifa vikifanya uhalifu mbaya unaojumuisha mauaji na uhalifu wa kingono. Bachelet ameitolea wito serikali ya Kongo kuwapa usalama watu wake badala ya kuchangia katika kuwanyanyasa.

''Kuwalinda raia ni jukumu la serikali, na serikali inapolipuuza jukumu hilo inaiweka jamii hatarini. Nchini DRC, uzoefu unatuonyesha kuwa matokeo yanaweza kuwa mabaya sana.'' Amesema Michelle Bachelet.

Msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu Marta Hurtado ameliambia shirika la habari la AFP kuwa tangu Septemba iliyopita, operesheni za kijeshi na ulipizaji kisasi dhidi ya raia vimewalazimisha watu 400,000 kuzihama nyumba zao katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kumejaa makundi ya wanamgambo yenye silahaPicha: Reuters/G. Tomsaevic

Wengine zaidi ya 110,000 wamekuwa wakimbizi wa ndani katika mkoa wa Kivu Kusini, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto. Machafuko katika mkoa wa Kivu Kusini yanaripotiwa kuongezeka sana kuanzia mwezi Machi mwaka huu.

ICC yaonya, yaazimia kupeleka ujumbe

Ripoti hii ya Umoja wa Mataifa imekuja siku moja baada Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu-ICC yenye makao yake mjini The Hague kusema inafuatilia kwa wasiwasi mkubwa ripoti za ghasia mpya kaskazini-mashariki mwa Kongo, na kuwa inapanga kutuma ujumbe wake huko hivi karibuni.

Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Fatou Bensouda kuna ripoti za kuaminika, kwamba makundi yenye silaha yanawashambulia raia katika eneo hilo na kuwauwa au kuwakata viungo.

Katika ghasia za hivi karibuni kabisa zilizotokea usiku wa Jumanne, watu 16, watano miongoni mwao wakiwa watoto, walichinjwa katika kijiji cha Mambisa, si mbali kutoka mji wa Bunia katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

 

AFP, APE

 

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW