1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaEthiopia

UN: Watu kadhaa wauawa katika mapigano katika eneo la Amhara

18 Novemba 2023

Umoja wa Mataifa umesema Ijumaa kwamba takriban raia 50 wameuawa katika mapigano na mashambulizi katika eneo la Amhara nchini Ethiopia katika muda wa mwezi mmoja uliopita

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed katika mkutano na waandishi wa habari mjini Rime Italia mnamo Februari 6, 2023
Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy AhmedPicha: Massimo Percossi/Ansa/ZUMA Press/IMAGO

Katika taarifa, msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Seif Magango, amesema kuwa ni muhimu kwa pande zote katika mzozo huo kujiepusha na mashambulizi yasiyo halali na kuchukua hatua zote muhimu kulinda raia.

Magango ameelezea wasiwasi wake kuhusu athari mbaya za mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na ghasia nyinginezo kwa wakazi katika eneo la Amhara huku kukiwa na mapigano yanayoendelea.

Soma pia:UN: Watu 183 wameuawa tangu mwezi Julai Amhara, Ethiopia

Magango ameliambia shirika la habari la AFP kwamba takriban watu 47 wameuawa katika mashambulizi matano tofauti tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba na kwamba wote walikuwa raia.

Katika hatua nyingine, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, ametoa tahadhari kuhusu ghasia hizo katika mazungumzo ya simu ya jana Ijumaa na waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed.

Msemaji wa wizara hiyo Matthew Miller, amesema kuwa  Blinken alisisitiza umuhimu wa mazungumzo katika kutatua migogoro.