1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres: Watu milioni 780 wanakabiliwa na njaa duniani

Hawa Bihoga
16 Oktoba 2023

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ni jambo la kuchukiza katika ulimwengu uliosheheni chakula, kuna mtu anakufa kwa sababu ya njaa kila baada ya sekunde chache.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Yuki Iwamura/AFP/Getty Images

Katika hotuba yake Guterres amesema dunia inaadhimisha siku ya chakula mwaka huu, huku kukishuhudiwa mzozo wa chakula, na ulimwengu ukirudi nyuma katika kukabiliana na tatizo la njaa na utapiamlo.

Amesema kiasi ya watu milioni 780 ulimwenguni kote wanakabiliwa na njaa huku karibu watoto milioni hamsini wapo katika hatari ya kupoteza maisha. Wakati ombi la ufadhili wa misaada ya kiutu kwa  miaka hii likiitikiwa kwa asilimia thelathini na mbili pekee.

Licha ya Guterres kuzitolea mwito serikali za nchi wanachama kuhakikisha zinaingilia kati mzozo wa chakula kwa watu wake, amesema bado zinakabiliwa na uhaba wa rasilimali. 

Soma pia:Ulimwengu waadhimisha Siku ya Chakula bila chakula

Amesema kuna umuhimu kwa serikali ulimwenguni kuchukua hatua ya kuhakikisha watu wanacho chakula cha kutosha.

"Hata hivyo serikali nyingi hazina rasilimali,"Alisema Guterres.

Aliongeza kuwa changamoto nyingi kwa mataifa kufikia lengo la kukabiliana na  njaa ni kutokana na serikali nyingi hazina rasilimali.

"Kuna umuhimu wa muitikio  wa kimataifa ili kukabiliana na mzozo wa chakula."

Ameongeza kwamba sababu ambazo zinachangia mzozo wa chakula ulimwenguni ni pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa yanayoshuhudiwa ulimwenguni, migogoro inayoendelea, kuyumba kwa hali ya uchumi pamoja na ukosefu wa hali ya usawa.

Viongozi: Chakula na Maji visitumike kama zana za vita

Kwa upande wake Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Fancis amesema, dunia inaadhimisha siku hii katika wakati ambapo idadi kubwa ya watu wamevunjika moyo na wanateseka kwa umasikini.

Kwa nini Afrika lazima iimarishe kilimo cha kisasa ?

01:52

This browser does not support the video element.

Hali hiyo ikiwa ni matokeo ya dhuluma na kukosekana kwa usawa ambao unawacha wachache wakiwa wanaishi katika maisha ya neema.

Akihutubia katika siku hii ya chakula kwenye jukwaa la Shirika la Chakula Duniani FAO Rais wa Italia Sergio Mattarella amesema ni uhalifu kutumia chakula na maji kama zana katika migogoro inayoendelea ulimwengu.

Aliongeza kwamba kupambana na njaa ni "kazi ya thamani kwa amani" na kwamba kuna haki ya chakula na maji "iliyoandikwa ndani ya haki pana zaidi ya kuishi" ya kila mwanadamu.

Soma pia:WFP yaanza kusambaza tena chakula Ethiopia

Alisema vita vimechangia hali ya kukosekana kwa utulivu katika maeneo mbalimbali ulimwenguni, hasa katika mataifa yalio hatarini hali ya uhaba wa chakula imeendelea kushuhudiwa na kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu.

 Kauli mbiu ya mwaka huu ya Siku ya Chakula Duniani inaangazia maji - hitaji la chakula chenye lishe na afya.