1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yabaini mauaji ya kikatili Burundi

21 Septemba 2016

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa waliokuwa wakifuatilia madai ya utesaji na mauaji yanayodaiwa kufanywa dhidi ya wapinzani wa serikali nchini Burundi wametoa orodha ya watuhumiwa wanaopaswa kushitakiwa.

Askari Polisi wakiwa katika doria mjini Bujumbura, Burundi
Askari Polisi wakiwa katika doria mjini Bujumbura, BurundiPicha: Getty Images/AFP

Jopo la wachungunguzi hao limethibitisha kiasi ya watu 564 waliouwa katika taifa hilo la Afrika ya kati katika kipindi cha mwaka 2015 wakati Rais Pierre Nkurunzinza alipokumbana na upinzani mara baada ya kutangaza kuwania muhula wa tatu wa uongozi.

Hata hivyo serikali ya Burundi imekanusha madai hayo yote na kusema ripoti hiyo imeegemea upande mmoja ikiwa na msukumo wa kisiasa.

Wachunguzi hao wamesema wamepokea ushahidi unaohusiana na vitendo vya kikatili vikiwemo vya ubakaji, kutoweka kwa watu katika mazingira ya kutatanisha, utesaji na mauaji na kuwa kunauwezekano kukawa na maelfu ya watu waliokumbana na hali hiyo ambapo wengi wao ni wale walionekana kupingana na hatua hiyo ya Rais Pierre Nkurunziza au wafuasi wa vyama vya siasa.

"Hakuna uhsahidi wa kutosha"

Baadhi ya mashahidi waliwataja maafisa 12 waandamaizi wa vyombo vya usalama wanaodaiwa kuhusika na kutoweka kwa baadhi ya watu waliokamatwa wakati wa kipindi cha machafuko hayo ya mwaka jana huku baadhi ya mashahidi wakidai kuteswa na kufichwa katika maeneo yaliyotengwa maalumu ikiwa ni pamoja na katika makazi ya Rais na Mawaziri.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo orodha ya watuhumiwa hao itakabidhiwa kwa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya haki za binadamu kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria pindi zitapohitajika.

"Mashitaka yaliyoibuliwa na wachunguzi hawa wa Umoja wa Mataifa yanamwelekeo wa kisiasa na yasiyokuwa na ushahidi uliothibitishwa," alisikika akisema Willy Nyamitwe ambaye ni msemaji wa ofisi ya Rais.

Kwa upande mwingine afisa mmoja wa ngazi ya juu katika jeshi la Burundi aliwaeleza wachunguzi juu ya orodha ya watu wanaopaswa kuondolewa katika orodha hiyo.

Serikali ya Burundi yakanusha madai hayo

Serikali ya Burundi imekanusha idadi hiyo ya watu waliouawa na kusema tuhuma hizo zimejengwa na watu wanaotaka kupandikiza hofu na kuleta mgawanyiko ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama nchini humo.

Msemaji wa serikali Burundi, Willy NyamitwePicha: DW/J. Johannsen

Aidha ripoti hiyo imesema miiili ya baadhi ya watu waliouawa ilisafirishwa kupitia mto Ruzizi na kuzikwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huku pia ikiorodhesha matukio ya ukatili dhidi ya haki za binadamu unaodaiwa kufanywa na maafisa wa usalama wa Burundi ikiwa ni pamoja na kuwalazimisha baadhi yao kukalia vioo vilivyo vunjika au mtu kulazimishwa kukaa jirani na nduguye aliyeuwa.

Wanawake waliolazimika kukimbia nchini humo na wale walionekana kuupinga utawala wa Rais Pierre Nkurunzinza walifanyiwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na vijana wanaounda kundi la vijana chini ya chama tawala nchini humo linalojulikana kama Imbonerakure.

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imeeleze pia kuwepo kwa picha zilizopigwa kutokea angani zinazo onyesha makaburi makubwa walimozikwa watu waliouawa wakati wa mauaji yanayodaiwa kutekelezwa na vyombo vya usalama nchini Burundi ambapo serikali haikuruhusu uchunguzi ufanywe katika maeneo yanakodaiwa kuwepo makaburui hayo.

Takribani watu 300,000 wameikimbia nchi hiyo na kuishi kama wakimbizi kufuatia machafuko yaliyoibuka nchini humo.

Wachunguzi hao wameonya kuwa iwapo hakutakuwa na mabadiliko katika serikali ya Burundi kuhusiana na muelekeo wa sasa wa siasa za nchi hiyo na pia Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua basi taifa hilo linaweza kutumbukia tena katika hali kama hiyo kwa mara nyingine.

Awali serikali ya Burundi iliripotiwa kuunda tume tatu kwa ajili ya kuchunguza madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu lakini hata hivyo Umoja wa Mataifa umeishutumu serikali ya nchi hiyo kwa kushindwa kufanya uchunguzi huo ipasavyo.

Mwandishi: Isaac Gamba/ RTRE

Mhariri: Iddi Ssessanga