UN yaeleza wasiwasi kuhusu machafuko Kaskazini mwa Msumbiji
7 Oktoba 2025
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) nchini Msumbiji, Xavier Creach, amesema katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, wameshuhudia mateso makubwa, huku raia wa kawaida wakilengwa moja kwa moja na mashambulizi.
UNHCR imeripoti kuwa zaidi ya watu 100,000 wamelazimika kuyakimbia makaazi yao tangu mwanzoni mwa mwaka huu, na takriban watu 22,000 walikimbia ndani ya wiki moja tu mwishoni mwa Septemba.
Mashambulizi mapya yameripotiwa katika miezi ya hivi karibuni katika jimbo la Cabo Delgado, ambako uasi unaoendeshwa na makundi yenye mafungamano na kundi linalojiita Dola la Kiislamu umeendelea tangu mwaka 2017.
Mwezi uliopita, waasi hao walishambulia bandari muhimu ya Mocimboa da Praia, wakipambana na vikosi vya serikali na kuwachinja raia, tukio lililozua hofu na kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi wa ndani.