1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yaelezea wasiwasi kuhusu mazingira ya hofu Venezuela

14 Agosti 2024

Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi kuhusu "mazingira ya hofu" baada ya uchaguzi nchini Venezuela, uliompa ushindi Rais Nichola Maduro, ambao wapinzani wanaupinga vikali.

Argentina waandamana mbele ya ubalozi wa Venezuela
Upinzani unaandamana kupinga matokeo yaliompa ushindi Rais Nicholas Maduro, ukisema mgombea wake alipata zaidi ya theluthi mbili ya kura.Picha: Esteban Osorio/Sipa USA/picture alliance

Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi kuhusu "mazingira ya hofu" baada ya uchaguzi nchini Venezuela, mnamo wakati wabunge nchini humo wanazingatia kupitisha sheria kadhaa ambazo wakosoaji wanasema zinawalenga wapinzani wa Rais Nicholas Maduro.

Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk, amesema katika taarifa jana kuwa anatatizwa na idadi kubwa na inayoongezeka ya ukamataji watu kiholela, pamoja na matumizi ya nguvu kupita kiasi, vinavyoripotiwa tangu kumalizika kwa uchaguzi, na mazingira yaliofuatia ya hofu.

Rais Nicolas Maduro akizungumza na wafuasi wake wakati wa mkutano wa serikali mjinicCaracas, Venezuela, Jumamosi, Agosti 3, 2024.Picha: Matias Delacroix/AP Photo/picture alliance

Soma pia:Maduro ahimiza 'mkono wa chuma" wa serikali kuzima maandamano 

Tume ya Uchaguzi ya Venezuela ilimtangaza Maduro kuwa mshindi kwa muhula wa tatu wa miaka sita, kwa kumpa asilimia 52 ya kura. Hata hivyo tume hiyo haijafafanua matokeo hayo.

Upinzani unasema hesabu zake za kura kutoka vituoni zinaonyesha Edmundo Gonzalez Urrutia, alishinda zaidi ya theluthi mbili ya kura. Marekani, Umoja wa Ulaya na mataifa kadhaa ya Amerika Kusini pia yamepinga madai ya Maduro ya ushindi.

Wakati huo bunge la nchi hiyo limeanza kujadili sheria kadhaa jana Jumanne, ambazo zitaiongezea makali miongozo ya usajili na ufadhili wa mashirika yasiyo ya kiserikali, baada ya spika wa bunge Jorge Rodriguez, ambaye ni mshirika wa Maduro, kuyataja mashirika hayo kama kiota cha kufadhili vitendo vya ugaidi.