1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yahimiza msaada zaidi Gaza baada ya kupitishwa azimio

23 Desemba 2023

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa wito wa kuongezwa msaada wa kiutu kwa watu wa Gaza. Hii ni baada ya Baraza la Usalama hatimaye kulipigia kura azimio kuhusu Gaza baada ya mabishano ya siku kadhaa

UN Sicherheitsrat zu Gaza
Picha: DAVID DEE DELGADO/REUTERS

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa wito wa kuongezwa msaada wa kiutu kwa watu wa Gaza, lakini mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema namna Israel inavyoendesha operesheni yake ya kijeshi inaweka vizuizi vikubwa katika usambazaji wa msaada katika ukanda huo uliozingirwa.

Soma pia: Azimio kuhusu vita vya Gaza kupigiwa kura

Baada ya siku kadhaa za mabishano ili kuepusha kitisho cha kura ya turufu ya Marekani, Baraza la Usalama jana Ijumaa lilipitisha azimio likihimiza hatua za kuruhusu "shughuli za kiutu kufanyika kwa njia salama, bila vikwazo" huko Gaza na kuwekwa "mazingira ya usitishaji endelevu" wa mapigano.

Hamas na Mamlaka ya Palestina yenye makao yake makuu katika Ukingo wa Magharibi wamegawanyika juu ya hatua hiyo. Hamas inasema azimio hilo halitoshi kukidhi mahitaji ya Gaza na linakaidi wito wa kimataifa wa kukomesha "uchokozi wa Israeli." Wizara ya Mambo ya Nje ya Mamlaka ya Palestina imeikaribisha hatua hiyo ikisema ni hatua itakayosaidia "kukomesha uchokozi, kuhakikisha kuwasili kwa msaada na kuwalinda watu wa Palestina."