1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yahimiza pande pinzani Libya kukubaliana kuhusu uchaguzi

28 Juni 2022

Mkuu wa masuala ya kisiasa wa Umoja wa Mataifa ameyahimiza makundi pinzani Libya kukubaliana kuhusu hatua zinazosimamia kipindi cha mpito kuelekea uchaguzi, wakati wa mazungumzo yanayofanyika wiki hii jijini Geneva

Schweiz Libysches Dialogforum in Genf
Picha: UNITED NATIONS/AFP

DiCarlo ameelezea matumaini kuwa hatua hiyo itasaidia kufanyika haraka iwezekanavyo uchaguzi uliosubiriwa kwa muda mrefu. Mkuu wa masuala ya kisiasa wa Umoja wa Mataifa Rosemary DiCarlo ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa wakati wa mazungumzo ya Cairo kuanzia Juni 12 hadi 20, pande pinzani za Libya zilifikia maelewano mapana kuhusu vifungu vingi tata katika katiba inayopendekezwa.

Soma pia: Pande hasimu Libya zashindwa kuafikiana juu ya uchaguzi

DiCarlo amesema mkutano huo wa Cairo ulikuwa wa kwanza kuona wajumbe wa bunge la Libya lenye makao yake mashariki mwa nchi, Baraza la Wawakilishi, na Baraza Kuu la Taifa lenye makao yake magharibi mwa nchi wakibadilishana maoni mazito kuhusu pendekezo la katiba tangu ilipoidhinishwa mwaka wa 2017.

Bashagha na Dbeibah wanaongoza serikali pinzani Libya

Afisa amelihimiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye nchi 15 wanachama na washirika wote wa kimataifa wa Libya kuwashinikiza viongozi wa mabunge yote mawili kuitumia fursa iliyojitokeza kufuatia makubaliano yaliyofikiwa Cairo na kufanikisha uchaguzi.

Mpango wa Libya kufanya uchaguzi Desemba 24 ulivunjika baada ya serikali ya mpito ya Tripoli, inayoongozwa na Abdul Hamid Dbeibah, kushindwa kundesha kura hiyo. Dbeibah alikataa kuwachia madaraka, akiibua maswali kuhusu mamlaka yake. Wabunge wa bunge la mashariki walijibu kwa kumchagua waziri mkuu pinzani Fathy Bashagha, aliyekuwa waziri mwenye nguvu wa mambo ya ndani anayeongoza serikali pinzani mjini Sirte.

Soma pia: Umoja wa Mataifa waongeza muda wa ujumbe wake Libya kwa miezi mitatu

Kwa upande wa kiuchumi, DiCarlo amesema sekta ya mafuta nchini Libya bado imefungwa kwa sehemu. "Tangu Aprili 16, kufungwa kwa visima vya mafuta kumepunguza mauzo ya nje ya mafuta ya Libya kwa thuluthi moja na kuigharimu nchi hiyo dola bilioni 3.1 katika hasara ya mapato. Aidha, ugomvi juu ya udhibiti na matumizi ya fedha za umma ambao ulichochea kufungwa kwa sehemu kwa visima bado unaendelea na huenda ukasababisha kufungwa kwa visima zaidi vya mafuta katika muda mfupi ujao"

Kamanda Khalifa Hifter alitangaza nia ya kugombea uraisPicha: picture-alliance/AP Photo/I. Sekretarev

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa juhudi za maridhiano, akionya kuwa migawanyiko ya kisiasa inayoendelea inachangia katika mazingira tete ya usalama ndani na nje ya mji mkuu Tripoli. Suala la afisa mkuu mtendaji wa Libya halijatatuliwa na ameonya kuwa wakati makundi ya wanamgambo yakijipanga kumuunga mkono Debeibah au Bashagha, kitisho cha kuongezeka machafuko kinakuwa kikubwa.

Baada ya mkutano wa Cairo, ripoti za vyombo vya habari vya Libya zilidai kuwa mada kuu iliyopingwa ni vigezo vya kugombea urais. Kwa mujibu wa ripoti, Baraza Kuu la Libya lenye makao yake mjini Tripoli lilisisitiza kuhusu kupigwa marufuku kiongozi wa kijeshi kugombea wadhifa wa ofisi ya juu ya nchi hiyo, hatua inayoonekana kumlenga Hifter, kiongozi wa kijeshi aliyetangaza nia yake ya kugombea katika uchaguzi wa Desemba, wakati wabunge wa bunge la mashariki wakitoa wito wa kuruhusu maafisa wa jeshi kugombea.

Soma pia:Kizungumkuti cha serikali mpya nchini Libya

Libya yenye utajiri wa mafuta imekumbwa na mzozo tangu vuguvugu lililoungwa mkono na NATO lilipomuondoa na kumuua aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu Muammar Gaddafi mwaka wa 2011. Nchi hiyo kisha ikagawanyika mara mbili na serikali pinzani, moja upande wa mashariki, ikiungwa mkono na kamanda wa kijeshi Khalifa Hifter na serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa katika mji mkuu Tripoli. Kila upande unaungwa mkono na wanamgambo tofauti na madola ya kigeni.

AP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW