UN yaidhinisha usitishwaji mapigano Syria
25 Februari 2018Kwa uungwaji mkono wa Urusi , Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinisha azimio kuhusu kusitisha mapigano ili kuruhusu upelekaji wa misaada ya kiutu pamoja na kuwaondoa wagonjwa na waliojeruhiwa, "bila kuchelewa".
Baada ya kura hiyo katika Baraza la Usalama, ndege za kivita za Syria zikisaidiwa na ndege za kivita za Urusi zilifanya mashambulio mapya katika mji huo wa Ghouta mashariki, limesema shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria.
Kiasi watoto 127 ni miongoni mwa watu 519 waliouwawa katika kampeni hiyo ya mashambulio ambayo utawala wa Syria ulianzisha Jumapili iliyopita dhidi ya eneo hilo la waasi, nje kidogo ya mji mkuu Damascus, shirika hilo la kuangalia haki za binadamu lenye makao yake mjini London lilisema.
Kiasi ya raia 41 waliuwawa katika mashambulizi ya jana Jumamosi(24.02.2018), ikiwa ni pamoja na watoto wanane. Urusi ilikana kushiriki katika mashambulizi hayo.
Macron na Merkel kuzungumza na Putin
Haraka kufuatia kura hiyo , Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wamesema watazungumza leo Jumapili (25.02.2018) na Rais wa Urusi Vladimir Putin kuhakikisha kwamba makubaliano hayo ya kusitisha mapigano yanatekelezwa "katika siku zinazokuja," Ikulu ya Ufaransa imesema katika taarifa.
Ufaransa na Ujerumani zilipambana kupata uungwaji mkono wa Urusi kwa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano nchini Syria , ambayo kwa kiasi kikubwa ni kuruhusu misaada kufika katika eneo hilo lililozingirwa na kuruhusu kuondolewa kwa watu.
Kura hiyo katika Umoja wa Mataifa awali ilitarajiwa kufanyika siku ya Alhamis, lakini ilicheleweshwa mara kwa mara wakati wanadiplomasia wakivutana katika majadiliano makali kuepuka kura ya veto ya Urusi , ambayo kijeshi inaiunga mkono serikali ya Rais Bashar al-Assad.
"Kila dakika ambayo baraza liliisubiria Urusi, madhila ya binadamu yaliongezeka," amesema balozi wa Marekani katika Umoja wa mataifa Nikki Haley baada ya kura hiyo, akiishutumu Urusi kwa kuzuwia.
Balozi wa Urusi Vassily Nebenzia alipuuzia shutuma hizo za kuburuza miguu, akisema kwamba majadiliano yalihitajika ili kufikia madai ya kusitisha mapigano ambayo "yatawezekana."
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Caro Robi