1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yaikosoa lugha chafu ya Trump kuhusu Afrika na Haiti

12 Januari 2018

Tume kuhusu Haki za Binadaamu katika Umoja wa Mataifa imesema ikiwa itathibitika kuwa Trump alitumia maneno hayo basi ni ya aibu na ubaguzi

Schweiz Rupert Colville
Picha: AFP/Getty Images

Umoja wa Mataifa umemshutumu rais wa Marekani Donald Trump kuhusiana na matamshi yake dhidi ya Haiti na nchi za bara la Afrika kuwa ni nchi za Uvundo. Umoja huo umesema matamshi hayo ni ya aibu na ya kibaguzi. Hata hivyo Donald Trump amekana kuwa hiyo si lugha aliyoitumia.

Msemaji wa Tume kuhusu Haki za Binadaamu katika Umoja wa Mataifa Rupert Colville amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa endapo itathibitika kuwa Trump aliyatumia maneno hayo dhidi ya Haiti na nchi za Afrika basi, ni maneno ya ubaguzi, yanayoshangaza na ya aibu kutolewa na rais wa Marekani.

Rupert Colville amesema huwezi kuzitusi nchi na mabara kuwa ya uvundo na kwa kuwa raia wao sio wazungu basi hawakaribishwi kwako. Pia amekosoa dhana kuwa Marekani inapaswa kuwapokea tu wahamiaji kutoka nchi kama Norway kwa vile ni Wazungu badala ya wahamiaji watokao Haiti au bara la Afrika.

Athari ya maneno hayo ni mbaya

Uganda ni kati ya nchi za Afrika ambazo zimeikosoa kauli ya TrumpPicha: Getty Images/Afp/Phil Moore

"Hili si suala tu kuhusu lugha chafu, ni kuhusu kufungua mlango kukaribisha maovu dhidi ya ubinadamu. Ni kuthibitisha na kueneza ubaguzi na woga ambao mwishowe utaharibu na kuvuruga maisha ya watu wengi. Hii pengine ni mojawapo ya athari na hatari mbaya zaidi itakayotokana na matamshi kama hayo kutoka kwa mwanasiasa wa ngazi ya juu."

Colville alikuwa akirejelea matamshi ya Trump wakati wa kikao na wabunge Alhamisi jioni kujadili mswada wa mageuzi kuhusu uhamiaji, pale alipohoji  ni kwa nini Marekani iwapokee wahamiaji kutoka katika nchi za uvundo kama Haiti na za bara Afrika badala ya kutoka nchi kama Norway.

Kauli ya Trump yakosolewa na nchi za Afrika

Matamshi ya Trump pia yamekosolewa na Umoja wa Afrika uliosema yanazua mgawanyiko na yanahujumu maadili ya ubinadamu duniani kote. Waziri wa mambo ya nje wa Uganda Henry Okello amesema ni matamshi ya kusikitisha na kujutia. Serikali ya Botswana imeyataja maneno ya Trump kuwa ya kibaguzi.

Nchi nyinginezo barani Afrika pia zimeanza kuyakosoa matamshi hayo. Jessie Duarte ambaye ni naibu katibu mkuu wa chama tawala nchini Afrika Kusini ANC amesema matamshi ya Trump ni ukosefu wa heshima wa kiwango cha juu.

Matamshi ya Trump ya hivi karibuni ni kati tu ya matamshi yake mengine ambayo yamewahi kuzusha hisia msetoPicha: picture alliance/AP/dpa/D.- J. Phil

"Yetu si nchi yenye uvundo vilevile Haiti, au nchi yoyote yenye shida. Ni makosa makubwa kwa Rais Trump kutoa matamshi hayo kuhusu nchi nyingine ambazo hazikubaliani na msimamo au sera zake katika mataifa hayo. Inasikitisha kuona anatoa kauli kama hizo."

Trump akana kutumia lugha chafu

Wakati akizidi kukosolewa, Trump ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa maneno hayo yaliyoripotiwa kwanza na jarida la Washington Post, siyo aliyoyatumia. Ikulu ya Marekani, haijayakana maneno hayo vilevile wabunge wa chama cha Republic waliokuwepo kwenye kikao hicho hawajayakanusha.

Kando na hayo, Trump ameifuta ziara yake ya London iliyopangwa kufanyika mwezi ujao, akimlaumu mtangulizi wake Barrack Obama kwa kuuza jengo la ubalozi wa zamani wa Marekani nchini humo kwa kiwango kidogo cha fedha.

Mwandishi: John Juma/AFPE/APE

Mhariri: Yusuf Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW