1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

UN yaishtumu Uganda kuwasaidia waasi wa M23

10 Julai 2024

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imesema jeshi la Uganda limetoa msaada kwa kundi la waasi wa M23 wanaoendesha uasi Mashariki mwa DR Kongo.

Uganda | Wanajeshi wa UPDF kwenye mpaka na Kongo
Wanajeshi wa Uganda wakilinda usalama kwenye upande wao wa mpaka na DR Kongo katika mji wa Bunagana, baada ya M23 kuchukuwa udhibiti wa upande wa Kongo mnamo mwaka 2023.Picha: Glody Murhabazi/AFP/Getty Images

Ugandaimekanusha kuhusika katika mzozo huo, ikisema inashirikiana kwa karibu na vikosi vya serikali ya Kongo. Kwa muda mrefu Umoja wa Mataifa umekuwa ukiishutumu Rwanda kuunga mkono kundi la M23, ambalo mara kadhaa limeteka ardhi kubwa ya eneo lenye utajiri wa madini mashariki mwa Kongo, madai ambayo Rwanda ilikanusha.

Kongo imekumbwa na vita kwa miongo kadhaa. Uganda na Rwanda ziliivamia mwaka 1996 na 1998 kwa kile walichosema ni kujilinda dhidi ya makundi ya wanamgambo wa ndani. Uganda bado inaendesha operesheni ya pamoja na wanajeshi wa Kongo dhidi ya kundi la waasi la Uganda, na Allied Democratic Forces,ADF.

Soma pia: Waasi wa M23 waendelea kukamata miji muhimu ya Kongo

Waasi wa M23 wanaoongozwa na Watutsi wamekuwa wakianzisha uasi mpya katika eneo la mashariki mwa Kongo linalokumbwa na uasi tangu 2022.

Vikosi vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, FARDC, vimekuwa vikiendesha operesheni ya pamoja na vile vya Uganda, UPDF, dhidi ya waasi wa ADF. Lakini UN yasema pia UPDF inawasaia waasi wa M23.Picha: Alain Uaykani/Xinhua/picture alliance

Wanajeshi wa Uganda walikuwa sehemu ya kikosi cha kikanda kilichotumwa mnamo Novemba 2022 kusimamia usitishaji mapigano na M23. Serikali ya Kongo ilitoa wito kwa kikosi hicho kuondoka mwaka jana, ikisema hakikuwa na ufanisi.

"Tangu kuzuka upya kwa mzozo wa M23, Uganda haijazuia kuwepo kwa wanajeshi wa M23 na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) kwenye ardhi yake au kupita humo," lilisema kundi la Wataalamu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika ripoti yao iliyotumwa kwa kamati ya vikwazo ya Baraza la Usalama mwishoni mwa Aprili na kisha kwa wajumbe wa Baraza la Usalama mwezi Juni.

Kundi hilo la Umoja wa Mataifa pia lilisema limepata ushahidi unaothibitisha uungaji mkono hai wa M23 na jeshi la Uganda na maafisa wa ujasusi wa kijeshi, huku viongozi wa M23, akiwemo Sultani Makenga aliyewekewa vikwazo, wakisafiri kwenda Uganda kuhudhuria mikutano.

Jeshi la Uganda lakanusha madai ya UN

Naibu msemaji wa jeshi la Uganda, Deo Akiiki, alisema katika mazungumzo na shirika la habari ya Reuters kuwa ripoti kama hizo zinalishutumu jeshi la nchi hiyo ya Afrika Mashariki wakati uhusiano wake na vikosi vya Kongo (FARDC) uko katika kiwango bora.

"Itakuwa uenda wazimu kwetu kuvuruga eneo lile lile tunalojitolea kila kitu kuhakikisha lina utaulivu," alisema Akiiki.

Ufafanuzi: Nani yupo nyuma ya mzozo wa Kongo?

02:01

This browser does not support the video element.

Ripoti hiyo ya UN ilisema wanajeshi 3,000-4,000 wa Rwanda walikuwa wakipigana upande wa waasi wa M23 dhidi ya jeshi la Kongo. "Udhibiti wa ukweli na mwongozo wa jeshi la Rwanda juu ya operesheni za M23 pia unaifanya Rwanda kuwajibika kwa hatua za M23," walisema wataalam wa Umoja wa Mataifa.

Soma pia: Tshisekedi azidi kutema cheche dhidi ya Rwanda, M23 washambulia tena Sake

Katika majibu yake, Rwanda ilisema Kongo ilikuwa ikifadhili na kupigana pamoja na waasi wa Kihutu, wa kundi la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR), ambao wameshambulia Watutsi katika nchi zote mbili.

"DRC ina uwezo wote wa kupunguza mzozo huu ikiwa wanataka, lakini hadi wakati huo Rwanda itaendelea kujilinda," msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo aliiambia Reuters.

Chanzo: Reuters

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW