UN yaitaka MONUSCO kusadia maandalizi ya uchaguzi DRC
28 Machi 2018Baraza la Usalama kwa sauti moja lilipitisha azimio lililowasilishwa na Ufaransa ambalo linarefusha muda wa ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini DRC MONUSCO, ambao ndiyo ujumbe mkubwa zaidi wa UN duniani, hadi Machi 2019, na kusisitiza haja ya kuwalinda raia wakati DRC ikijiandaa na uchaguzi wa kihistoria mwezi Desemba.
Mataifa ya Magahribi yanazidisha shinikizo kwa rais Kabila kuruhusu makabidhiano ya amani ya madaraka baada ya kura ya Desemba 23 na kudhibiti vikosi vyake vya usalama baada ya dazeni kadhaa za watu kuuawa katika maandamano ya kumpinga.
Urusi ilionya kuwa wanajeshi wa kulinda amani hawapaswi kuchukuwa upande katika uchaguzi huku balozi wa DRC akisema ujumbe huo unapaswa kujikita katika kupambana na makundi ya waasi -- na siyo kusaidia uchaguzi.
Uchaguzi kwa utulivu na amani
Balozi wa Ufaransa Francois Delattre alisema uchaguzi huo ni muhimu kwa mustakabali wa DRC lakini pia kwa kanda nzima, ukisafisha njia ya makabidhiano ya kwanza kabisaa ya amani ya madaraka katika historia ya taifa hilo. "Bila uchaguzi wa kuaminika na wote, utulivu wa nchi na kanda nzima utakuwa hatarini," aliliambia baraza baada ya kura.
Serikali mjini Kinshasa imepanga tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo lakini Kabila, alieko madarakani tangu 2001, hajabainisha wazi iwapo ataachia madaraka, na kuzusha hofu kwamba nchi hiyo itatumbukia katika vurugu kubwa.
Azimio la baraza la usalam "linatilia mkazo haja y akufanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba uchaguzi unaandaliwa katika mazingira ya uwazi, uaminifu na ushirikishwaji, na usalama."
Baraza lilimuomba klatibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kufanya mipango ya kuimarisha ujumbe wa kulinda amani ikiwa itahitajika, "kwa kuzingatia njia zote" kama vile kutuma vikosi vya ziara kutoka ujumbe mwingine wa Umoja wa Mataifa. Guterres ataripoti kwa baraza hilo ndani ya siku 90 kuhusu mpango wa dharura.
Chini ya azimio hilo, MONUSCO itatoa msaada wa kiufundi na lojistiki za uchaguzi, kusaidia kuwapa mafunzo askari polisi wa Kongo na kufuatilia ukiukaji wa haki za binadamu ambavyo utaripoti kwa baraza.
Urusi, China zatahadharisha
Ikitoa tahadhari, Urusi ilisisitiza kuwa mamlaka ya ujumbe huo ilikuwa kuwalinda tu raia na siyo kujiingiza katika masuala ya ndani ya taifa hilo huku China ikisema uhusu wa DRC laazima uheshimiwe.
"Ni muhimu kuepuka kikamilifu hali ambako MONUSCO inaweza kuunga mkono moja ya pande za Kongo huku vurugu za uchaguzi zikiwa pia zinaendelea," alisema balozi wa Urusi Dmitry Polyanskiy.
Jumuiya ya kimataifa inapaswa kuusaidia uongozi wa Kongo "kuimarisha uwezo wake wa kiusalama ili uweze kuleta utulivu katika taifa hilo kwa uhuru," alisema balozi wa China Wu Haitao.
Balozi wa DRC katika Umoja wa Mataifa Ignace Gata Mavita alipingana na uamuzi wa baraza hilo, akisema mamlaka ya ujumbe huo inapaswa "kupambana na makundi yneye silaha ili kuwalinda raia na kurejesha amani na usalama mashariki mwa nchi yetu." Balozi huyo alirejelea wito wake kwa MONUSCO kuondolewa DRC baada ya karibu miaka 20.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/AFPE
Mhariri: Josephat Charo.