1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yalia na ukiukaji mkubwa, na mauaji Burundi

Mjahida 15 Januari 2016

Mkuu wa kitengo cha haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu madai ya vikosi vya usalama kushiriki matendo maovu ya ubakaji wa wanawake, mauaji na kuwazika watu katika makaburi ya halaiki, katika mgogoro wa Burundi.

Schweiz UN-Menschenrechtsrat Said Raad al-Hussein
Mkuu wa kitengo cha haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad Al HusseinPicha: picture-alliance/dpa/M. Trezzini

Afisa huyo Zeid Ra'ad Al Hussein ameonya katika taarifa yake kwamba, dalili zote ikiwemo mauaji yanayochukua muelekeo wa kikabila zinaashiria hali ya hatari. Zeid ameendelea kuonya kuwa mwenendo mpya unaotia wasiwasi unaibuka katika mgogoro wa Burundi ukiwemo visa vya udhalilishwaji wa kingono unaodaiwa kufanywa na vikosi vya usalama.

Zeid Ra'ad ameongeza kuwa hali inasemekana kuwa sawa katika visa vyote, vikosi vya usalama vinadaiwa kuingia majumbani kwa waathiriwa kuwatenganisha wanawake na familia zao kisha kuwabaka na katika matukio mengine kuwabaka wanawake hao kwa makundi.

Polisi na jeshi pia wanadaiwa kuwakamata kiholela vijana wengi ambao waliteswa, kuuwawa au kuchukuliwa na kupelekwa mahali pasipojulikana.

Baadhi ya wanajeshi wa Burundi wakiwabeba vijana waliyokamatwa mjini BujumburaPicha: Getty Images

Mkuu huyo wa kitengo cha haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa sasa ametaka uchunguzi wa haraka na wa dharura kufanyika juu visa vya mauaji vilivyotokea mwezi uliopita mjini Bujumbura na madai ya watu walioshuhudia makaburi ya halaiki yapatayo tisa ndani na nje ya mji huo, ikiwemo kambi moja ya kijeshi inadaiwa kuwa na zaidi ya miili 100 ya watu waliouwawa mnamo Desemba tarehe 11.

Zeid amesema Ofisi yake bado inaangalia picha za satellaiti katika juhudi za kugundua mengi zaidi juu ya madai yaliyotolewa.

Wataalamu wa masuala ya haki za binaadamu kupelekwa Burundi

Kwa upande wake mtaalamu wa masuala ya haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Afrika, Scott Campbell amesema kundi la wataalamu watatu liko tayari kupelekwa Burundi kuchunguza makaburi ya halaiki yanayodaiwa kuwepo wakati wa mgogoro unaoendelea lakini hadi sasa serikali ya Burundi haijatoa idhini ya kundi hilo kuingia nchini humo.

Baadhi ya mauaji yanayofanyika mjini Bujumbura, BurundiPicha: Reuters/J.P. Aime Harerimana

Tangu mapigano yalipoanza nchini Burundi mwezi Aprili watu 439 wameuwawa huku maelfu wengine wakiyakimbia makaazi yao na kuingia nchi jirani kutokana na hofu ya kuongezeka mapigano.

Burundi iliingia katika mgogoro wa kisiasa baada ya rais Pierre Nkurunziza kutangaza mwezi Aprili azma yake ya kuwania tena kiti cha urais na mgogoro ukashamiri zaidi baada ya rais huyo kushinda uchaguzi wa mwezi Julai mwaka jana.

Mwandishi Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Gakuba Daniel