UN yamuondolea vikwazo Rais Sharaa wa Syria
7 Novemba 2025
Azimio hilo lililoandaliwa na Marekani na kupitishwa jana Alhamisi pia limemuondolea vikwazo Waziri wa Mambo ya Ndani wa Syria Anas Khattab. Liliidhinishwa kwa kura 14, lakini China ilijizuia.
Washington imekuwa ikiwarai wanachama 15 wa baraza hilo kuilegezea Syria vikwazo. Na mnamo mwezi Mei, Rais Donald Trump alitangaza mabadiliko makubwa ya kisera kuelekea taifa hilo, aliposema ataiondolea vikwazo.
Baada ya kuidhinishwa, Trump alimsifu Sharaa kwa kufanya kazi nzuri na hatua kubwa imepigwa nchini humo licha ya mazingira magumu.
"Tutakutana... Na nadhani anafanya kazi nzuri sana. Ni mazingira magumu Na yeye ni mtu mahiri. Lakini ninaelewana naye vizuri sana, na hatua kubwa imepigwa kuhusu Syria. Hilo ni jambo gumu, lakini hatua kubwa imepigwa. Tuliondoa vikwazo kwa ombi la Uturuki na Israel," Trump aliwaambia waandishi wa habari.
HTS iliwekewa vikwazo tangu 2014
Baada ya miaka 13 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, Rais Bashar al-Assad alifurushwa mnamo mwezi Disemba kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na vikosi vilivyoasi vikiongozwa na kundi la Islamist Hayat Tahrir al-Sham (HTS).
Kundi hilo ambalo awali lilitambulika kama Nusra Front, lilikuwa ni tawi rasmi la kijeshi la kundi la kigaidi la al Qaeda nchini Syria hadi pale lilipovunja uhusiano mwaka 2016. Tangu Mei, 2014, kundi hilo lilikuwa chini ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa vilivyolenga makundi ya al Qaeda na lile linalojiita Dola la Kiislamu, IS.
Wafuasi wengi wa HTS pia wanakabiliwa na vikwazo hivyo, kuanzia kuzuiwa kusafiri, mali zao kuzuiwa hadi vizuizi vya silaha. Lakini sasa Sharaa na Khattab wako huru.
China yalipinga azimio la UN
Hata hivyo China ilijizuia kupiga kura kwa kuwa ilisema azimio hilo halikuelezea kwa kina juu ya namna suala la ugaidi litakavyoshughulikiwa pamoja na hali ya usalama nchini Syria, hii ikiwa ni kulingana na Balozi wa China kwenye Umoja wa Mataifa Fu Cong.
China kwa muda mrefu imekuwa ikielezea wasiwasi wake kuhusiana na mustakabali wa Vuguvugu la itikadi kali la Eastern Turkistan Islamic Movement (ETIM) huko nchini Syria, ambalo wanamgambo wa Uyghur kutoka China na Asia ya Kati ni wafuasi wake. Na makundi ya haki za binaadamu yamekuwa yakiishutumu Beijing kwa kuinyanyasa jamii hiyo ya walio wachache.
Hata hivyo Fu amesema azimio hilo limeweka wazi kwamba Syria inapaswa "kuchukua hatua madhubuti za kupambana na vitendo vya kigaidi" na kushughulikia kitisho cha wanamgambo wa kigeni wa makundi ya kigaidi, ambayo ni pamoja na vuguvugu hilo la ETIM lililoko nchini Syria.
Balozi wa Urusi kwenye Umoja huo Vassily Nebenzia kwa upande wake amesema Moscow inaunga mkono azimio hilo kwa sababu ya umuhimu wake na imetanguliza maslahi na matarajio ya watu wa Syria.
Urusi ilimlinda kidiplomasia mshirika wake Assad wakati wa vita, ikipiga kura ya turufu zaidi ya mara kumi na mbili katika Baraza la Usalama, mara nyingi ikiungwa mkono na China wakati Baraza hilo lilipokutana mara kadhaa kujadili hali ya kisiasa na kibinadamu nchini Syria