1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yaomba dola bilioni 3.85 kuepusha balaa Yemen

25 Februari 2021

Umoja wa Mataifa umewatolea mwito wahisani na hasa mataifa ya Kiarabu jirani na Yemeni kuisadia nchini hiyo inayokabiliwa na mzozo mbaya zaidi wa kiutu, kwa kuchangia kiasi cha dola bilioni 3.85 ili kuepusha maafa.

Jemen Kinder im Flüchtlingslager in der Provinz Hajjah
Picha: picture-alliance/Photoshot/M. Al Wafi

Umoja wa Mataifa unasema Yemen inakabiliwa na baa kubwa la ukosefu wa chakula na  njaa na inahitaji dola bilioni 3.85 kukabiliana na hali hiyo. Mkuu wa  shughuli za kibinadamu katika  Umoja wa Mataifa Mark Lowcock amezitaka nchi za ulimwengu na hasa Saudi Arabia na Umoja wa falme za Kiarabu kujitowa kuisaidia nchi hiyo.

Yemen iko vitani kwa kipindi kirefu na hivi sasa inaelekea ukingoni kutumbukia katika janga kubwa la njaa  ambalo halijawahi kushuhudiwa duniani kwa miongo kadhaa,ikiwa nchi wafadhili na hasa zile nchi jirani za Ghuba hazitoonesha ukarimu wa kuisadia nchi hiyo. Umoja wa Mataifa unaomba msaada wa dola bilioni 3.85 kwa ajili ya Yemen.

Saudi Arabia na Umoja wa falme za kiarabu ambazo zilionesha ukarimu mkubwa na kuchangia mwaka 2018 na 2019 baada ya Umoja wa Mataifa kuomba msaada kwa ajili ya nchi hiyo zimetakiwa kwa mara nyingine kutochoka kuonesha ukarimu wao mara hii baada ya mwaka jana kuacha ghafla kuchangia.

Mvulana wa Kiyemeni akipokea msaada wa kiutu uliyotolewa na shirika la Chakula Duniani, WFP mjini Taiz, Oktoba 10, 2020.Picha: AHMAD AL-BASHA/AFP/Getty Images

Hatua ya kukosekana msaada huo ilichangia mashirika ya msaada kupunguza idadi ya wanaowapa msaada wa chakula na misaada mingine nchini Yemen. Mwaka jana ni raia milioni 9 tu waliokuwa wakipewa msaada huo kutoka idadi ya watu milioni 13 hadi 14 waliokuwa wakipewa msaada huo kila mwezi mnamo mwaka 2019.

Lowcock mkuu wa shughuli za kibinadamu wa Umoja wa Mataifa aamesema watu milioni 4 waliokosa msaada wa chakula mwaka jana ni miongoni mwa wale wanaosubiri rehma na wanaokabiliwa na kitisho cha kufa kutokana na njaa. Maelezo hayo ya Lowcock ameyatowa katika mkutano na waandishi habari kwa njia ya vidio katika wakati ambapo Jumatatu ijayo kunatarajiwa kufanyika mkutano wa kuchangisha fedha kwa ajili ya Yemen utakaongozwa kwa pamoja na Sweden na Uswizi ambapo katibu mkuu Antonio Guterres  atatangaza ombi la kuchangishwa bilioni 3.85.

Ameonya Lowcock,kwamba bila ya fedha hizo kupatikana basi watu wengi zaidi watakufa na huenda likashuhudiwa janga kubwa sana katika nchi hiyo ya kiarabu.Amesisiza kwamba hali ni mbaya na kuna dharura ya suala hilo kuchukuliwa hatua. Yemen nchi masikini kabisa duniani imeharibiwa kwa kiwango cha kutisha na vita vilivyoanza mwaka 2014 pale waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran walipouteka na kuudhibiti mji mkuu Sanaa na sehemu kubwa ya kaskazini mwa nchi hiyo.

NAibu Katibu Mkuu wa UN anaeshughulikia masuala ya kiutu Mark Lowcock.Picha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Hii ndiyo iliyokuwa chachu ya kujiingiza nchini humo muungano wa kijeshi wa nchi za Kiarabu ulioongozwa na Saudi Arabia pamoja na  Emarati,na ukiungwa mkono na Marekani. Muungano huo wa kijeshi ulijiingiza kwenye vita hiyo kusaidia kuirudisha madarakani serikali ya rais Abed Rabu Mansour Hadi.

Hivi sasa kwa mujibu wa LowCock mkuu wa shughuli za msaada za Umoja wa Mataifa,sera mpya kuelekea Yemen ya serikali ya rais Joe Biden ambayo inalenga kumaliza vita hivyo vya miaka sita na kusitisha uungaji mkono wa muungano huo wa kijeshi wa nchi za kiarabu inatowa fursa kubwa ya kupatikana amani na maendeleo nchini Yemen,na hasa kutokana na jinsi Saudi Arabia ilivyoipokea sera hiyo.Mpaka sasa mgogoro wa Yemen umewaondoa duniani kiasi watu 130,000 na kuacha balaa kubwa la mgogoro wa kibinadamu.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Gakuba, Daniel

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW