UN yaonya kuhusu 'ukatili wa kutisha' nchini Sudan
31 Oktoba 2025
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wameonya kwamba hali inayoendelea nchiniSudan ni ya ukatili mkubwa na ni kitisho kikubwa kutokana na mashambulizi yanayoendelea ya vikosi vya wanamgambo wa RSF.
Hivi karibuni mji waEl-Fasher uliopo katika jimbo la Darfur uliangukia mikononi mwa RSF. Mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Tom Fletcher amesema eneo hilo kwa sasa linakabiliwa na maafa makubwa na mateso ya kibinadamu yasiyoelezeka.
Kukamatwa kwa mji wa El Fasher kunakuja baada ya zaidi ya miezi 18 ya kuzingirwa na kuzua hofu ya kurejea kwa ukatili uliolenga makabila miaka 20 iliyopita.
Fletcher ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba mauaji hayafanyiki Darfur pekee na kwamba kuna umwagaji mkubwa wa damu unaoendelea pia katika jimbo la Kordofan na hivyo kuhatarisha shughuli za utoaji misaada kwa raia wa Sudan.