1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yaonya kuhusu watoto wakimbizi kukosa elimu

20 Novemba 2018

Umoja wa Mataifa umesema nchi zinazowapokea wakimbizi hazifanyi juhudi za kutosha kuwaingiza watoto wakimbizi katika mifumo yao ya elimu na kwamba juhudi zaidi zinahitajika ili kuwajumuisha watoto hao ulimwenguni kote.

Pressebild LBS Kinderbarometer
Picha: LBS

Hayo yameelezwa kwenye ripoti ya elimu iliyotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO mjini Berlin, Ujerumani. Ripoti hiyo iliyopewa jina 'Ufuatiliaji wa Elimu Ulimwenguni mwaka 2019'', imeonya kuwa watoto wengi wakimbizi bado wananyimwa elimu bora.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nusu ya watu waliolazimika kuyakimbia makaazi yao wana umri chini ya miaka 18 na mara nyingi hawana uwezo wa kujiunga na mifumo ya elimu katika nchi wanazoenda kuomba hifadhi.

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Audrey Azoulay amesema kuwa elimu ni muhimu na kwamba watu hawatoweza kusonga mbele kama elimu kwa wahamiaji na wakimbizi haipewi kipaumbele.

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Audrey Azoulay Picha: picture-alliance/dpa/Chen Yichen

Kwa upande wake Manos Antoninis, mkurugenzi wa ripoti hiyo ya elimu amezionya nchi kutodhani kwamba kazi inakamilika pindi wahamiaji wanapoingia shule. Amesema wanakuwa wakitengwa kwa njia nyingine nyingi.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa ukosefu wa walimu wenye ujuzi na fedha vimekuwa vikikwamisha juhudi za kuwaingiza shuleni wanafunzi wahamiaji.

Aidha, ripoti hiyo imefafanua kuwa Ujerumani pekee inahitaji walimu wapya 42,000 kwa ajili ya kuwafundisha watoto wakimbizi waliochukuliwa kama sehemu ya sera ya Kansela Angela Merkel ya kufungua milango kwa wakimbizi iliyoanza mwaka 2015.

Nchi za Afrika zapongezwa

Chad, Ethiopia na Uganda zimepongezwa kwa kuwaandikisha wakimbizi katika shule zao, zikiwa katika kundi la nchi zenye kipato cha chini, huku Canada na Ireland zikipongezwa kwa kutekeleza sera za elimu jumuishi, katika mataifa yaliyoendelea kiviwanda na yale yanayoinukia.

Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani, Gerd Müller amesema nchi yake itaongeza fedha kwa ajili ya elimu ya vijana katika matukio ya dharura kama vile vita, kutoka Euro milioni 16 hadi milioni 31.

Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani, Gerd MüllerPicha: picture-alliance/dpa/C. Koall

Müller amesema kiasi ya watoto milioni 75 walioko katika mazingira yenye mizozo, hawana uwezo wa kupata elimu, hivyo juhudi zinahitajika, la sivyo watoto hao watakuwa hawana malengo wala matarajio.

Ukweli ni kwamba ukosefu wa walimu wa kufundisha masomo ya utangamano na lugha, kunamaanisha kuwa watoto wakimbizi wako katika hatari ya kuacha shule mara mbili zaidi ya wanafunzi wa nchi hizo katika nchi za Umoja wa Ulaya.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa nchi zenye kipato cha chini na cha wastani zinawahifadhi asilimia 89 ya wakimbizi, lakini zinakabiliwa na ukosefu wa fedha kwa ajili ya kuwapatia elimu. Aidha, ripoti hiyo imetoa wito kwa wafadhili kuongeza msaada wa kifedha kwa mara tatu zaidi na kuhakikisha msaada huo wa elimu ya wakimbizi ni wa muda mrefu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, AFP, DW, https://bit.ly/2BidLEf
Mhariri: Caro Robi