1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

UN yaonya uwezekano wa janga la kiutu al Fashir

Angela Mdungu
17 Mei 2024

Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa mataifa Volker Turk amesema amefedheheshwa na vurugu zinazozidi kuongezeka karibu na mji wa al Fashir nchini Sudan.

Darfur
Uharibifu katika soko la wanyama al Fasher kutokana na machafukoPicha: AFP

Volker amewatahadharisha makamanda wanaohusika na mzozo unaoendelea karibu na mji huo wa al Fashir juu ya janga la kibinadamu linaloweza kutokea.

Mkuu huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa mataifa Volker Turk amesema tayari ameshafanya majadiliano na makamanda wa pande mbili zinazohasimiana nchini Sudan. Ameelezea wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa kuibuka kwa janga la kibinadamu kama mji wa al Fashir utashambuliwa.

Soma zaidi: UN: Mapigano ya silaha nzito mjini El-Fasher nchini Sudan

Amewaambia makamanda hao kuwa mapambano katika mji huo ambao zaidi ya wakazi milioni 1.8 na watu waliokimbilia mjini hapo kutokana na mapigano wanaishi, na wako katika hatari ya njaa yanaweza kusababisha maafa. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva msemaji wa Turk, Ravina Shamdasani, amearifu kuwa Turk amesema mapigano katika eneo hilo yatazidisha mzozo baina ya jamii na kusababisha matokeo mabaya kwa raia.

UN: Misaada ya kiutu bado inahitajika Sudan

Katika hatua nyingine, Umoja wa mataifa umesema umepokea asilimia kumi na mbili tu ya dola bilioni 12, kwa ajili ya kuisaidia Sudan, iliyoathiriwa vibaya na vita wakati baa la njaa likizidi kuijongea. Akizungumzia hilo, msemaji wa ofisi ya uratibu wa masuala ya kiutu ya Umoja wa mataifa OCHA bwana  Jens Laerke ametanabaisha kuwa, bila ya misaada zaidi kutolewa haraka, mashirika ya misaada yatashindwa kuwasaidia watu wanaokabiliwa na njaa na kuzuia maafa zaidi.  Zaidi, Laerke ametoa wito kwa wafadhili  kutimiza ahadi zao.

Raia wasio na makazi wakiwa katika kambi ya wakimbizi ya Abu Shouk karibu na al Fashir Picha: AFP

Soma zaidi:UN: Sudan inakabiliwa na ghasia na uhaba wa misaada 

Kulingana na msemaji huyo, nusu ya idadi ya watu wa Sudan wanahitaji msaada wa kiutu. Katika siku za hivi karibuni, Umoja wa Mataifa umekuwa ukionesha wasiwasi kuhusu ripoti za mapigano makali katika maeneo yenye watu wengi wakati kundi la RSF likipambana  kuudhibiti mji wa El-Fasher. Mji huo ndio eneo pekee la Darfur magharibi lisilo chini ya kundi hilo.

Maelfu ya watu wameuawa na mamilioni wamelazimika kuyahama makazi yao katika taifa hilo, tangu vilipoibuka vita mnamo mwezi April mwaka 2023 kati ya jeshi linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah Burhan dhidi ya kikosi cha RSF chini ya Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW