UN yapinga wapalestina kuhamishwa Gaza
9 Julai 2024Israel imetanua onyo lake kwa maeneo mengine mengi ya Ukanda wa Gaza, ikitaka wakazi wa maeneo hayo kuondoka mara moja ili iendelee na operesheni yake ya kuwaangamiza wanamgambo wa Hamas.
Tangu tarehe 27 Juni, Israel imetoa amri tatu za Wapalestina kuondoka katika mji wa Gaza na katika eneo la kusini la mji huo. Tayari shirika la Umoja wa Mataifa limekadiria kuwa maelfu ya Wapalestina wameshautoroka mji.
Wakaazi waliobakia huko wameripoti kusikia milio ya makombora na ufyatulianaji risasi pamoja na kuona ndege za helikopta angani usiku kucha katika maeneo ya Kusini Magharibi mwa Gaza.
Ofisi ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa, imeshitushwa na amri ya Israel kutaka Wapalestina waondoke makwao ikisema tayari watu hao wamepoteza makaazi yao mara kadhaa kuelekea katika maeneo ambayo pia jeshi la Israel linaendelea kushambulia na raia pia kuendelea kuuwawa na kujeruhiwa.
Jeshi la Israel laushambulia vikali Ukanda wa Gaza
Jeshi la Israel limesema linapambana na ugaidi unaofanywa na Hamas huku likisema tayari limeshawauwa wanamgambo kadhaa, kupitia mashambulizi ya angani na ardhini na kukamata silaha za wanamgambo hao.
Hamas: Mashambulizi huenda yakasambaratisha mazungumzo ya amani
Hamas nayo imejibu na kusema mashambulizi hayo yaliyosababisha mauaji ya Wapalestina 18, yanatia doa mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza, yanayotarajiwa kuanza kesho 10.07.2024 nchini Qatar.
Kiongozi wake Ismail Haniyeh amesema mashambulizi hayo yanaweza kurudisha nyuma juhudi za mazungumzo hayo na mchakato mzima kuanza upya.
Haniyeh amedai Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anajaribu kwa maksudi kuyasambaratisha mazungumzo hayo kwa kuimarisha mashambulizi ya jeshi lake Gaza.
Kiongozi wa Hamas azungumza na wapatanishi kuhusu usitishaji vita Gaza
Huku hayo yakiarifiwa wapatanishi wa Misri na Qatar wanaoungwa mkono na Marekani wameendeleza juhudi zao wiki hii za kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano ya Gaza na kuachiwa kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas na pia kurejea kwa wafungwa wa Kipalestina wanaozuwia nchini Israel.
Mkuu wa shirika la ujasusi la Marekani, CIA, William Burns na mwenzake wa shirika la Ujasusi la Israel la Mosad, David Barnea wanatarajiwa kusafiri kueleka doha kesho kwa mazungumzo hayo na pia kukutana na Waziri Mkuu wa Qatar.
afp/ap/reuters