1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yatambua utumwa kama uhalifu wa kihistoria

26 Machi 2026

Uamuzi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wafungua ukurasa mpya wa majadiliano kuhusu fidia, uwajibikaji na uponyaji wa kihistoria.

New York 2026 |
Ingawa si azimio la kisheria, lina uzito wa kisiasa na linaashiria mwelekeo mpya wa dunia katika kukabiliana na majeraha ya kihistoria.Picha: Lev Radin/ZUMA/IMAGO

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio linalotambua kuwa biashara ya utumwa dhidi ya Waafrika ni "uhalifu mbaya zaidi dhidi ya ubinadamu” na kuzitaka nchi zilizohusika kulipa fidia kama hatua thabiti katika kurekebisha makosa ya kihistoria.

Azimio hilo, lililowasilishwa na Ghana, limeitaka dunia kutambua rasmi kuwa biashara ya utumwa wa kuvuka Bahari ya Atlantiki—iliyodumu kwa zaidi ya karne tano na kusababisha mamilioni ya Waafrika kutekwa, kuuzwa na kufa—ndilo tukio lenye athari pana zaidi katika historia ya ubinadamu. Hata hivyo, pendekezo hilo limepitishwa licha ya upinzani mkali kutoka baadhi ya mataifa ya Ulaya na Marekani.

Katika kura ya Baraza Kuu lenye wanachama 193, mataifa 123 yaliunga mkono azimio hilo, huku Marekani, Israel na Argentina zikilipinga, na nchi 52—ikiwemo Uingereza na Umoja wa Ulaya—zikijizuia kupiga kura. Ingawa si azimio la kisheria, lina uzito wa kisiasa na linaashiria mwelekeo mpya wa dunia katika kukabiliana na majeraha ya kihistoria.

Ghana imeeleza kuwa athari za utumwa bado zinaonekana leo kupitia tofauti za kiuchumi, kijamii na kimfumo zinazowakumba watu wenye asili ya Afrika. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana, Samuel Okudzeto Ablakwa amesema:

"Azimio hili linatuma ujumbe ulio wazi kabisa kwamba jumuiya ya kimataifa haitavumilia tena kutokuwajibika; kwamba jumuiya ya kimataifa inasimama upande wa haki; na kupitia mfumo wetu wa ushirikiano wa kimataifa tulioujenga, haijalishi itachukua muda gani, siku ya uwajibikaji itafika. Hivyo basi, sisi sote kama viongozi tunapaswa kuwa makini na matendo na sera zetu— Kwangu mimi, huo ni ujumbe mzito sana ambao Umoja wa Mataifa inautuma kwa dunia leo.”

Majadiliano na msamaha

Aidha azimio hilo linatoa mwongozo wa majadiliano kuhusu fidia, likihimiza mataifa kutoa msamaha wa wazi, kurejesha mali za kitamaduni zilizoibwa, kutoa fidia ya kifedha, na kuhakikisha mifumo ya ubaguzi haitokei tena. Pia linahimiza ushirikiano kati ya Umoja wa Afrika, mataifa ya Karibiani na taasisi za kimataifa katika kujenga mfumo wa pamoja wa marekebisho.

Kwa mara ya kwanza, Baraza Kuu limeweka kumbukumbu rasmi kwamba maumivu ya utumwa hayapaswi kusahaulika.Picha: Bianca Otero/ZUMA/picture alliance

Hata hivyo, baadhi ya mataifa ya Magharibi yameeleza wasiwasi kwamba azimio hilo linaweza kuonekana kama kuweka viwango tofauti vya makosa dhidi ya ubinadamu. Umoja wa Ulaya umeonya kuhusu changamoto za kisheria, hasa kuhusu kutekeleza sheria za sasa kwa matukio ya kihistoria.

Pamoja na changamoto za kisiasa na mitazamo tofauti, azimio hili limepokelewa kama ishara ya matumaini,  kwa dunia kukabiliana na historia kwa uaminifu, kutafuta njia za kurejesha haki, na kujenga mustakabali unaotambua utu wa kila binadamu.

Kwa mara ya kwanza, Baraza Kuu limeweka kumbukumbu rasmi kwamba maumivu ya utumwa hayapaswi kusahaulika—na kwamba safari ya uponyaji inaweza kuanza kupitia majadiliano, uwazi na hatua za pamoja.

UN kutambua biashara ya utumwa kuna tija kwa Afrika?

04:35

This browser does not support the video element.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW