1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yapunguza mgao wa chakula Yemen kutokana na ukata

Hawa Bihoga
22 Desemba 2021

Shirika la mpango wa chakula la umoja wa mataifa WFP limesema litapunguza mgao wa chakula kwa watu milioni nane nchini Yemen kuanzia mwezi Januari, kutokana na upungufu wa fedha.

Jemen Hilfe Katastrophenhilfe Flüchtlinge Flucht
Picha: AHMAD AL-BASHA/AFP/Getty Images

Taarifa iliyotolewa na shirika hilo la mpango wa chakula imeeleza kuwa familia ambazo zipo kwenye orodha ya kupata msaada wa chakula zitapata takriban nusu ya mgawo ambayo ndio kiwango cha chini kinachotolewa na WFP.

Misaada mingine ambayo itakuwa mashakani kukumbwa na changamoto hiyo ni pamoja na miradi ya kupambana na utapiamlo kwa watoto.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo hilo la mpango wa chakula WFP yalionya mapema mwaka huu juu ya uwezekano wa kupunguza shughuli zake kutokana na kupokea kiasi cha fedha kisichokidhi mahitaji.

Umoja wa Mataifa umeonya juu ya kupunguza zaidi mgao wa chakula Yemen ikiwa hali itaendelea kuwa mbaya.Picha: Khaled Abdullah/REUTERS

Soma pia: Waasi 40 wa Houthi wauwawa kwenye mapigano Yemen

Wafadhili wamechangia kiasi cha dola bilioni 2.68 hadi kufikia mwezi Oktoba, badala ya kiasi cha dola bilioni 3.85 zilizohizajika kufikia malengo ya programu za mashirka hayo.

Katika taarifa yake mkurugenzi wa kanda wa WFP  Corinne Fleischer, amesema akiba ya WFP nchini Yemen inapungua kwa kasi sana na kila mara wanavyopunguza chakula  wanafahamu kuwa watu wengi ambao tayari wana shida na uhaba wa chakula wataungana na kundi la mamilioni ambao wanakufa njaa.

Watu wapatao milioni tano ambao wapo katika hatari kubwa zaidi ndio watasalia na mgao kamili kutoka katika shirika hilo la Umoja wa Mataifa ambalo limekuwa likitoa msaada wa chakula nchini Yemen.

WFP imeongeza kuwa  hadi sasa inalisha takriban watu milioni 13 kwa mwezi katika taifa hilo la Mashariki ya Kati.

Kitisho cha baa la njaa

Yemen iliyogawanyika kati ya kundi la Houthi lenye mfungamano na Iran iliopo kaskazini mwa nchi hiyo  na serikali inayotambulika kimataifa iliyo upande wa kusini mwa nchi, imetumbukia katika baa la njaa kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka saba sasa.

Yemen imekumbwa na vita tangu mwaka 2016.Picha: Murad Abdo/Xinhua News Agency/picture alliance

Soma pia: Saudi Arabia na vita visivyo mwisho Yemen

Sababu ya hali hiyo ni pamoja na mfumuko mkubwa wa bei unaosababishwa na kushuka kwa thamani ya fedha pamoja na vikwazo vya uagizaji bidhaa kutoka nje.

Vita hivyo vimeua maelfu ya watu wengi wao wakiwa ni raia na kuwaacha mamilioni katika baa la njaa.

Mnamo mwezi Juni, WFP ilianza tena kutoa misaada ya chakula ya kila mwezi katika baadhi ya maeneo yanayodhibitiwa na Wahouthi ikiwa ni baada ya kupunguza ugawaji wa kila mwezi kutoka Aprili 2020 kutokana na wafadhili kuacha kutoa fedha.

Tayari Benki ya Dunia imeidhinisha kiasi cha dola milioni 170 kama msaada kwa Yemen kwa ajili ya miradi ya misaada ya chakula vijijini, miundombinu na mazingira.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW