1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yasema Ethiopia imewakamata madereva wake 70

10 Novemba 2021

Umoja wa Mataifa umesema mamlaka nchini Ethiopia zimewakamata madereva 70 walioajiriwa na umoja huo na mashirika mengine ya misaada, tangu serikali ilipotangaza hali ya hatari kufuatia kuongezeka kwa kitisho cha vita.

Äthiopien Tigray Konflikt l Gedenkgottesdienst für die Opfer mit Premier Abiy Ahmed Ali
Picha: Ethiopian Prime Ministry Office/AA/picture alliance

Taarifa ya leo ya Umoja wa Mataifa imesema UN inatafuta sababu za kukamatwa kwa watu hao, tangu Novemba tatu katika mji wa Semera, ambao ndiyo njia ya misafara ya msaada inayopelekwa mkoani Tigray, chini ya kile ambacho Umoja wa Mataifa umekielezea kuwa sawa na mzingiro wa kiutu. 

Siku ya Jumanne, takribani dazeni mbili za wafanyakazi wa Kiethiopia kutoka mashirika tofauti ya Umoja wa Mataifa walikamatwa bila kutolewa sababu katika mji mkuu wa Addis Ababa, na kwa mujibu  wa Umoja wa Mataifa, 16 kati yao wanasalia korokoroni.

Soma pia: Amnesty: Wapiganaji wa Tigray walibaka, kupora na kuwapiga wanawake

Tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Novemba, kumekuwa na ongezeko la ripoti za watu kutoka mkoa wa Tigray kukamatwa au kutekwa.

Msemaji wa serikali ya Ethiopia Legesse Tulu.Picha: Solomon Muchie/DW

Msemaji wa serikali Legesse Tulu ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba wafanyakazi 16 wa UN walikamatwa kwa sababu ya kushiriki katika ugaidi usiyohusiana na kazi, bila hata hivyo kutoa ufafanuzi. Serikali inasema inawakamata watu wanaoshukiwa kuviunga mkono vikosi vya Tigray.

Ethiopia imo katika mzozo mkali kati ya kundi la ukombozi wa watu wa Tigray, TPLF, na vikosi vya serikali, mzozo ambao umegharimu maelfu ya maisha na kuzusha madai ya uhalifu wa kivita.

Msuguano waongezeka na Umoja wa Mataifa

Mzozo huo umesababisha msuguano kati ya Umoja wa Mataifa na serikali ya waziri mkuu Abiy Ahmed, ambaye alituzwa nishani ya amani ya Nobel mwaka 2019, kutokana na mchango wake katika kurejesha amani na taifa jirani la Eritrea.

Soma pia: Makundi 9 yaunda muungano kumpinga Abiy

Wiki chache zilizopita, wafanyakazi saba wandamizi wa Umoja wa Mataifa walitimuliwa kutoka Ethiopia, katika hatua isiyo kifani, ambayo katibu mkuu wa umoja huo Antonio Guterres, alisema ilikiuka sheria ya kimataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anasema hatua ya Ethiopia kuwafukuza na kuwakamata watumishi wa umoja huo ni ukiukaji wa sheria ya kimataifa.Picha: Loey Felipe/UN Photo/Xinhua/picture alliance

"Tunalaani wazi wazi hatua iliyopita ya kufukuzwa kwa maafisa wa UN kutoka Ethiopia, na iwapo itathibishwa, tutalaani kukamatwa kwa wafanyakazi wa UN kwa misingi ya ukabila," alisema msemji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Ned Price.

Ethiopia, taifa la wakaazi milioni 115 wa makabila tofauti, linakabiliwa na kitisho cha kusambaratika baada ya mzozo huo kuidhoofisha serikali ya Abiy.

Mapigano yamesambaa katika maeneo mengine ya nchi baada ya kuanzia mkoani Tigray mwaka mmoja uliyopita.

Hivi leo, TPLF inaukaribia mji mkuu Addis Ababa, ikiwa pamoja na waasi kutoka kundi jengine lajeshi la ukombozi wa Oromo, OLA.

Ethiopia yatangaza hali ya hatari

01:20

This browser does not support the video element.

Chanzo: Mashirika