1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

UN yasema idadi kubwa walipigwa risasi kituo cha msaada Gaza

2 Machi 2024

Timu ya Umoja wa Mataifa imeripoti kuona "idadi kubwa" ya majeraha ya risasi miongoni mwa raia wa Gaza baada ya wanajeshi wa Israel kufyatua risasi karibu na msafara wa misaada.

Ukanda wa Gaza | Wanaume wakibeba mwili baada ya shambulio la Israel
Mwanamume akilia wakati mwili wa jamaa yake ukibebwa kwenda kuhifadhiwa baada ya shambulio la Israel kwenye msururu wa kupokea misaada.Picha: AFP/Getty Images

Rais wa Marekani Joe Biden alisema Ijumaa kuwa jeshi lake litaanza kudondosha misaada kutokea angani katika eneo hilo la Palestina ambako Israel inapambana na wapiganaji wa vuguvugu la Hamas linaloungwa mkono na Iran.

Siku ya Jumamosi wizara ya afya katika eneo hilo linaloongozwa na Hamas ilisema maelfu ya watu kaskazini mwa Gaza "wako katika hatari ya kufa kutokana na upungufu wa maji mwilini na utapiamlo", na Shirika la Afya Ulimwenguni lilisema limetoa matibabu kwa watoto 50 wenye utapiamlo mbaya kaskazini.

Wizara hiyo siku ya Ijumaa iliripoti jumla ya watoto 10 walikufa kwa "utapiamlo na upungufu wa maji mwilini". Wanajeshi wa Israel walifyatua risasi wakati raia wa Palestina wakihaha kutafuta chakula katika tukio la machafuko mjini Gaza siku ya Alhamisi ambapo wizara ilisema kuwa watu 115 waliuawa na zaidi ya 750 kujeruhiwa.

Jeshi la Israel lilisema "mkanyagano" ulitokea wakati maelfu ya wananchi wa Gaza walipouzingira msafara wa misaada, na kusababisha makumi ya vifo na majeruhi, ikiwa ni pamoja na baadhi ya waliokanyagwa. Chanzo cha habari cha Israel kilikiri kuwa wanajeshi waliufyatulia risasi umati huo, wakiamini kuwa "ni tishio".

Msemaji wa jeshi la Israel, Admiral Daniel Hagari, alisema wanajeshi walifyatua "risasi chache za onyo" kujaribu kutawanya "kundi la watu" ambalo "lilivamia" malori ya misaada.

Picha kutoka kwenye video ikionesha namna vikosi vya Israel vilivyowalenga Wapalestina, walipokuwa wamelizunguuka roli la misaada ya kiutu.Picha: Stringer/Anadolu/picture alliance

Vifo hivyo vya msafara wa misaada viliongeza idadi ya waliofariki katika vita vya Palestina huko Gaza hadi 30,320, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kulingana na wizara ya afya ya Gaza, inayoendeshwa na Hamas.

Vita hivyo vilianza Oktoba 7 kwa shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa la Hamas kusini mwa Israel na kusababisha vifo vya takriban watu 1,160, wengi wao wakiwa ni raia, kulingana na takwimu za Israel.

Siku ya Ijumaa timu ya Umoja wa Mataifa iliwatembelea baadhi ya waliojeruhiwa kutokana na tukio la msaada, katika Hospitali ya Al-Shifa ya Mji wa Gaza, na kuona "idadi kubwa ya majeraha ya risasi", msemaji wa mkuu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema.

Soma pia:Israel yauwa Wapalestina zaidi ya 100, yajeruhi zaidi ya 700

Hospitali hiyo ilipokea 70 kati ya waliofariki, na karibu majeruhi 200 walikuwa bado pale wakati wa ziara ya timu hiyo, msemaji Stephane Dujarric alisema.

Hakuwa na taarifa kuhusu timu inayowachunguza waliouawa, lakini alisema "kwa walivyoona wagonjwa waliokuwa hai wakipata matibabu ni kwamba kulikuwa na idadi kubwa ya majeruhi ya risasi".

Hossam Abu Safiya, mkurugenzi wa Hospitali ya Kamal Adwan ya Gaza City, alisema majeruhi wote iliowapokea walipigwa "risasi na makombora kutoka kwa vikosi vya ukaliaji", akimaanisha Israeli.

Uingereza ilijiunga na miito ya kimataifa ya uchunguzi, huku waziri wa mambo ya nje David Cameron akisema Israel ina "wajibu wa kuhakikisha kuwa misaada zaidi ya kibinadamu inawafikia" Wagaza.

Katika mahojiano yaliyochapishwa Jumamosi katika gazeti la Le Monde, mwenzake wa Ufaransa Stephane Sejourne alisema "dhamana ya kuzuiwa kwa misaada ni wazi kuwa inabebwa na Israel".

Sejourne alisema hali ya "janga" ya kibinadamu "iliunda hali zisizoweza kutetewa na zisizo na uhalali ambazo Waisraeli wanawajibika."

UN: Njaa haizuwiliki tena Ukanda wa Gaza

Jens Laerke, msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu OCHA, alisema siku ya Ijumaa kuwa "njaa imekuwa jambo lisiloepukika" Gaza endapo mambo hayatabadilika.

Laerke alitoa mfano wa kukaribia kufungwa kwa uagizaji wa chakula cha kibiashara, "msururu wa malori" yanayokuja na msaada wa chakula, na "vizuizi vikubwa kuhusu kusafiri ndani ya Gaza.

Watoto katika Ukanda wa Gaza wakipokea msaada wa chakulaPicha: Abed Zagout/Anadolu/picture alliance

Umoja wa Mataifa umetaja hasa vikwazo vya upatikanaji wa maeneo ya kaskazini mwa Gaza, ambako wakazi wamegeukia kula chakula cha mifugo na hata majani.

Hisham Abu Eid, 28, kutoka eneo la Zeitun Mjini Gaza, alisema alipata magunia mawili ya unga kutoka kwa usambazaji wa misaada na akawapa majirani zake moja.

"Kila mtu anakabiliwa na njaa. Misaada inayoingia Gaza ni adimu na haitoshi hata idadi ndogo ya watu. Njaa inaua watu," Abu Eid alisema. Mashahidi siku ya Jumamosi waliliambia shirika la habari la AFP kwamba mapigano ya bunduki yalitokea Zeitun.

Biden alisema Washington itaanza utoaji wa misaada kutokea angani "katika siku zijazo". "Tunahitaji kufanya zaidi, na Marekani itafanya zaidi," alisema, akiongeza pia "atasisitiza" Israeli kuruhusu malori zaidi ya misaada.

Soma pia:WHO yaonya kuhusu mashambulizi mapya ya Israel huko Rafah

Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji ilisema ukweli kwamba udondoshaji wa ndege "unazingatiwa ni ushahidi wa changamoto kubwa za ufikiaji Gaza".

Lakini shirika hilo lilisema ushushaji wa misaada kwa miamvuli sio suluhu na huvuruga "muda na juhudi za suluhu zilizothibitishwa kusaidia kwa kiwango kikubwa".  

IRC ilitoa wito wa "usitishaji endelevu wa mapigano" na vivuko vya ardhi kuingia Gaza vifunguliwe ili kusaidia usafirishaji.

Jordan yaongoza mfumo wa udondoshaji misaada

Jordan ilitangaza kwa mara ya kwanza kudondosha misaada mnamo Novemba na imefanya misheni nyingi tangu wakati huo, pamoja na Ufaransa na Uholanzi. Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu pia zimeanza kufanya kazi kwa pamoja kwenye udondoshaji wa angani.

Picha za AFPTV zilionyesha watu wakikimbia na kuendesha baiskeli kwa kasi wakipita majengo yaliyoharibiwa na mabomu kwenye barabara ya vumbi ili kufikia misaada inayoelea hadi katika Jiji la Gaza.

Samantha Power, ambaye anaongoza Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani, alisema wastani wa malori 96 ya misaada yalikuwa yakiingia Gaza kila siku -- ikiwa ni "sehemu tu ya kile kinachohitajika".

Mwandishi wa habari wa shirika la aliripoti mashambulizi kadhaa ya anga pamoja na mashambulizi ya mizinga wakati wa usiku mjini Rafah kusini mwa Gaza pamoja na mji wa Khan Yunis ulioko kilomita chache kaskazini, kitovu cha mapigano ambapo jeshi la Israel lilisema operesheni zinaendelea.

Msafara mwingine wa malori ya misaada waingia Gaza

01:57

This browser does not support the video element.

Soma pia:Israel yaitwanga Gaza kabla ya kura ya usitishaji vita UM

Wapatanishi wamekuwa wakijaribu kupata usitishaji mapigano na Biden alisema Ijumaa "anatumai" bado makubaliano yanaweza kufikiwa kabla ya mwezi mtukufu wa Waislamu wa Ramadhani, ambao unatarajiwa kuanza Machi 10 au 11.   

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu yuko chini ya shinikizo la ndani kuwarejesha nyumbani mateka 130 ambao Israel inasema wamesalia Gaza baada ya kukamatwa Oktoba 7, idadi hii ikiwa ni pamoja na 31 wanaodhaniwa kuuawa.

Tawi la kijeshi la Hamas lilisema Ijumaa kuwa mateka wengine saba wamefariki kutokana na operesheni za kijeshi za Israel, tangazo ambalo AFP halikuweza kulithibitisha kwa uhuru.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW