1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yasema mapigano Sudan yawaangamiza 91 El Fasher

2 Oktoba 2025

Umoja wa Mataifa umesema mashambulizi yaliyofanywa na wanamgambo wa RSF ndani ya siku 10 mwezi uliopita katika mji uliozingirwa wa El Fasher nchini Sudan yaliwauwa watu 91.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk
UN yasema mapigano ya wenyewe kwa wenyewe Sudan yamewaangamiza 91 El Fasher Picha: Uncredited/AP/dpa/picture alliance

Haya ni mashambulizi ya hivi karibuni kutokea ya vita kati ya  jeshi la taifa na wanamgambo wanaotaka kuudhibiti mji huo.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk, amesema eneo jirani na mji huo la Daraja Oula umekuwa ukishambuliwa mara kwa mara na RSF kupitia mashambulizi ya droni na ya ardhini kati ya Septemba 19 na 29.

Türk ametaka hatua za haraka kuchukuliwa ili kuzuwia mateso na mashambulizi ya kikabila mjini El Fasher. Wanamgambo hao hadi sasa bado hawajatoa maoni yoyote kuhusiana na taarifa hiyo.

Kulingana na takwimu shirika la afya ulimwenguni WHO, mapigano ya wenyewe kwa wenyewe Sudan kati ya RSF na jeshi la taifa yalioanza mwaka 2023 yamesababisha mauaji ya watu 40,000 huku wengi zaidi ya milioni 2 wakiachwa bila makao.