1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

UN yasema msaada usio na kikomo wahitajika Gaza

27 Oktoba 2023

Umoja wa Mataifa umeonya leo Ijumaa kwamba watu wengi zaidi watakufa katika Ukanda wa Gaza kutokana na mzingiro unaoendelea wa Israel, na kusisitiza kuwa huduma za msingi katika ardhi ya Palestina zimesambaratika.

Israel Jerusalem | Preseskonferenz UNRWA-Generalkommissar  - Philippe Lazzarini
Kamishna mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, Philippe Lazzarini (Mwanaume) akizungumza na wanahabari huko Jerusalem: 27.10.2023Picha: Mostafa Alkharouf/Anadolu/picture alliance

Kamishna mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, Philippe Lazzarini amesema watu wa Gaza wanakufa sio tu kutokana na mashambulizi ya mabomu, bali wengi watakufa kutokana na matokeo ya kuzingirwa kwa  Ukanda wa Gaza  huku huduma za msingi zikiathirika pakubwa na kukishuhudiwa uhaba wa dawa, chakula na maji. Aidha Lazzarini amesema mitaa ya Gaza sasa imejaa maji taka na kwamba hilo ni hatari:

"Gaza iko kwenye ukingo wa hatari kubwa ya kiafya, na hatari ya magonjwa inakaribia." Kinachohitajika ni mtiririko wa maana na usiokatizwa wa misaada. Na ili kufanikiwa hili, tunahitaji usitishaji mapigano kwa sababu za kibinadamu ili kuhakikisha msaada huu unawafikia wale wanaouhitaji."

Wafanyakazi wa Shirika la Umoja wa MAtaifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA wakiandaa msaada wa vifaa vya matibu huko Deir Al-Balah, kabla ya kusambaza bidhaa hizo katika hospitali za Gaza:25.10.2023Picha: Ashraf Amra/Anadolu/picture alliance

Hata hivyo, misaada ya kibinaadamu imeendelea kuwasilishwa, ambapo hapo jana malori kumi na mawili zaidi yaliyosheheni maji ya kunywa, chakula na bidhaa nyingine yaliwasili Gaza. Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, kabla ya shambulio la kigaidi la Hamas nchini Israel  7 Oktoba, takriban malori 500 ndiyo yaliyokuwa yakivuka mpaka kila siku kuingia huko Gaza.

Israel yaendeleza mashambulizi Gaza

Kulingana na wizara ya Afya inayodhibitiwa na kundi la Hamas, watu 481 wameuawa katika kipindi cha saa 24 zilizopita. Kwa mujibu wa mamlaka huko Gaza na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA), hadi sasa jumla ya Wapalestina 7,028 wameuawa tangu kuanza kwa mzozo huu Oktoba 7 huku  asilimia 66 kati yao wakiwa ni wanawake na watoto.

Soma pia:Ulaya yataka eneo salama la kibinaadamu kuundwa Gaza 

OCHA imetoa pia tathmini ya uharibifu ambapo imesema asilimia 45 ya nyumba zote katika Ukanda wa Gaza zimeharibiwa ikiwa ni sawa na nyumba 150,000 ama zilizoharibiwa au kutoweza tena kukaliwa.

Moshi ukidhihirika huko Gaza baada ya mashambulizi ya anga ya Israel: 27.10.2023Picha: Ali Jadallah/Anadolu/picture alliance

Jeshi la Israel limesema kundi la Hamas huficha zana zao za kijeshi katika majumba ya raia. Jeshi hilo limebainisha kwamba linajaribu kadri iwezekanavyo kuepusha majeruhi ya raia na kusisitiza kuwa hutoa onyo ya kuwataka raia kuondoka kabla ya mashambulizi ya roketi.

Kulingana na vyombo vya habari vya Urusi, Abou Hamid ambaye ni miongoni  mwa viongozi wa kundi la Hamas walioko ziarani mjini Moscow, amesema mateka wa Israel kamwe hawatoachiwa huru hadi kutakapofikiwa makubaliano ya usitishwaji mapigano  na kusisitiza kuwa mazingira tulivu yanahitajika ili kukamilisha zoezi hilo. Hapo jana kundi la Hamas lilisema karibu mateka 50 tayari wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel.