UN yashutumu mateso ya Urusi kwa wafungwa wa Ukraine
23 Septemba 2025
Umoja wa Mataifa umesema katika ripoti yake kwamba mamlaka za Urusi zimewatesa wafungwa wa kiraia katika maeneo inayoyakalia nchini Ukraine, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji mkubwa wa kingono ulioratibiwa.
Katika ripoti mpya, ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imehitimisha kwamba, Urusi tangu kuanza kwa uvamizi wake kamili wa Ukraine mnamo Februari 2022 imewaweka wafungwa raia wa Ukraine katika mifumo thabiti ya ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa.
Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa waliwahoji jumla ya raia 216 walioachiliwa kutoka kizuizini katika maeneo yaliyoshikiliwa tangu Juni 2023. Mnamo Mei 2025, mamlaka ya Ukraine iliripoti kwamba karibu raia 1,800 wa Ukraine walikuwa wakizuiliwa na Urusi, ikisisitiza kwamba idadi halisi inaweza kuwa kubwa zaidi.