UN yataka pande zinazohasimiana Yemen kushiriki mazungumzo
24 Juni 2020Vita vya Yemen vimesababisha mauaji ya zaidi ya watu 10,000 na wengine milioni mbili kukosa makaazi, katika janga baya zaidi la kibinaadamu duniani kwa wakati huu. Akizungumza katika mahojiano na shirika la habari la Associated Press, Guterres amesema watu wa Yemen tayari wanateseka sana na kwamba janga la COVID-19 linaifanya hali yao kuwa ngumu zaidi.
Kauli hiyo aliitoa jana kabla ya mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Martin Griffiths kuliarifu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika mkutano wa faragha kuhusu hali ya Yemen baadae leo.
Juhudi za kuwaleta pamoja mahasimu
Gutteres amesema Umoja wa Mataifa umekuwa ukifanya kazi kuzileta pamoja pande zinazohasimiana na kuendeleza hatua za kujenga uwezo wa kuaminiana katika masuala yanayohusiana na uwanja wa ndege, bandari, malipo ya mishahara na wakati huo huo kuanza kwa mchakato wa kisiasa na kuongeza kwamba bado anaamini hilo litawezekana.
Amebainisha kuwa wanahitaji kuongeza shinikizo kwa pande zinazohusika katika mzozo pamoja na wahusika wote muhimu ili kuhakikisha kwamba mazungumzo magumu yaliyofanyika kuhusu suala hilo yanaelekea katika kuleta matokeo mazuri.
Mwezi uliopita, Griffiths alielezea ''maendeleo makubwa'' yaliyofikiwa katika mazungumzo hayo kuelekea kwenye mpango wa kusitisha mapigano, lakini akaonya kuhusu changamoto kubwa kama vile kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya corona kwa kiwango kisichojulikana kwenye taifa hilo masikini la Kiarabu.
Tofauti zitatuliwe
Mjumbe huyo maalum aliuhimiza muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia na waasi wa Houthi kutatua haraka tofauti zao kuhusu hatua za kibinaadamu na kiuchumi zinazohitajika ili kuendeleza juhudi za amani na kuisaidia Yemen kupambana na virusi vya corona.
Wanadiplomasia wamesisitiza kwamba mpango wa amani wa Yemen lazima uipatanishe sio tu serikali na waasi wa Houthi, lakini pia eneo la kusini na kaskazini. Siku ya Jumatatu muungano huo wa kijeshi ulitangaza kuwa hatua imepigwa katika upande wa kusini.
Mwaka 2014, waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran waliudhibiti mji mkuu wa Yemen, Sanaa na eneo kubwa la kaskazini mwa nchi hiyo, na kusababisha serikali ya Rais Abed Rabbo Mansour Hadi kukimbilia uhamishoni.
Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia na kuungwa mkono na Marekani, uliingilia kati mwaka uliofuata kujaribu kuurejesha madarakani utawala wa Hadi. Hata hivyo, vita vya Yemen vimekwama na kusababisha mataifa muhimu ya eneo hilo kutafuta njia ya kujitoa.
(AP)