UN yaitaka Sudan Kusini kuharakisha uchaguzi uliocheleweshwa
18 Aprili 2024Matangazo
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliandika katika ripoti kwamba, ni muhimu vyama kuchukua hatua za dharura katika kufanikisha uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika.
Sudan Kusini haijafanya uchaguzi tangu ilipojinyakulia uhuru wake kutoka Sudan mwaka 2011, na taifa hilo linakumbwa na mizozo sugu, umaskini na majanga ya asili.
Soma pia:Viongozi wa Sudan Kusini wameshindwa kuandaa uchaguzi
Mipango ya uchaguzi imevurugwa na mabishano makali baina ya Rais Salva Kiir na adui wake mkuu, Makamu wa Rais Riek Machar. Vikosi vinavyowatii wapinzanihao wawili vilipigana vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe kati ya 2013- 2018 ambavyo vilisababisha vifo vya takriban watu 400,000 na mamilioni kukimbia makazi yao.