UN yataka vita Yemen vichunguzwe kimataifa
25 Agosti 2016Vita hivyo tayari vimekwisha wauwa maelfu ya watu, na kamisheni hiyo imesistiza kwamba jopo lililoundwa hapo awali nchini humo kuchunguza dhuluma hizo, limeshindwa kukidhi haja.
Mohammad Ali Alnsour, mkuu wa idara ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa, akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva leo hii ambapo aliwasilisha wito wa, Zeid Ra'ad al -Hussein, mkuu wa Ofisi ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa wakati ofisi yake hiyo ikitowa ripoti ya kura 22 yenye kuorodhesha dhila zinazofanywa na pande zote mbili katika mzozo huo ambao unazipambanisha serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa ikiungwa mkono na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya waasi wa Kishia wanaojulikana kama Wahouthi na washirika wao.
"Tunahitaji kuona uwazi zaidi kuhusiana na chunguzi hizi. Kulipwa fidia kwa wahanga ni kipengele muhimu lakini sio kipengele pekee. Nafikiri kunapaswa kuwepo kwa uwajibikaji fulani ili kwamba dhuluma hizi zisirudiwe tena," amesema Alnsour.
Katika taarifa yake, ofisi hiyo ya Zeid imetowa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuanzisha chombo huru cha kimataifa kufanya uchunguzi huru nchini Yemen, hususan ikitilia maanani changamoto zilizokabiliwa na jopo la taifa lililoundwa na Rais Abed Rabbo Mansour Hadi, hasa masuala ya usalama.
Kunahitajika ripoti isiyo na upendeleo
Alnsour, amesema ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na jopo hilo la taifa imelenga matumizi ya nguvu yaliofanywa na Wahouthi tu, wakati kunahitajika ripoti itakayokuwa haina upendeleo na kabambe zaidi juu kuvunjwa kwa haki za binaadamu kunakofanywa na pande zote mbili za mzozo huo. Amewaambia waandishi wa habari kwa bahati mbaya hali nchini Yemen ni mbaya sana.
"Kama tulivyotaja katika ripoti hiyo, pande zote mbili zinahusika zinalenga vituo vya raia vinavyolindwa kwa mijibu wa sheria ya kimataifa kama vile masoko, sherehe za harusi, mahospitali na vituo vyengine ambavyo vyote kwa kweli vinalindwa chini ya sheria ya ubinaadamu na vina ulinzi maalum wa kisheria," ameongeza Alnsour.
Zeid, mkuu wa ofisi ya haki za binaadamu katika Umoja wa Mataifa ambaye ni miongoni mwa wana familia ya kifalme nchini Jordan, hakuainisha jopo hilo la kimataifa la uchunguzi litaundwa na nani, lakini anatarajiwa kuwasilisha ripoti ya utafiti wake katika kikao cha Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa mwezi ujao.
Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binaadamu yanakadiria kwamba watu 9,000 kwa jumla wameuwawa tokea kuanzishwa kwa mashambulizi hayo ya anga hapo mwezi wa Machi 2015. Takriban watu milioni 3 wamepotezewa maskani ndani ya nchi hiyo ya kimaskini kabisa duniani.
Mwandishi: Mohamed Dahman/AP/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef