UN yataka Waarabu waisaidie Syria
6 Aprili 2017Akizungumza wakati wa ziara yake nchini Kuwait, ili kutia saini makubaliano ya msaada wa dola milioni 10 kwa wakimbizi wa Syria walio nchini Iraq, Naibu Kamishna Mkuu wa UNHCR, Kelly T Clements, alisema hakuna matumaini yoyote ya vita vya Syria kumalizimika karibuni. Clements alisema ni jambo la kuhuzunisha kuwa idadi ya wakimbizi waliokimbia vita nchini Syria kufikia sasa ni zaidi ya millioni 5. Mkuu huyo wa shirika la UNHCR aliongeza kuwa hawajaona suluhisho lolote la kisiasa ili kuhakikisha raia wa Syria wanarejea nyumbani salama na kwa hiari.
Kupitia kwa msemaji wa shirika hilo la UNHCR, Babr Baloch, Clements alisema: "Tangu mwezi Februari mwaka huu, zaidi ya wakimbizi elfu 47 wamekimbia vita na uharibifu nchini Syria. Uturuki hivi sasa imewapatia makaazi karibu wakimbizi millioni tatu. Ndio maana UNHCR kwa mara nyingine tena inaomba jumuiya ya kimataifa, mataifa wafadhili na hata watu binafsi kuyasadia mataifa kama Uturuki, Lebanon na mengine mengi yaliyo eneo hilo, ambayo yameubeba mzigo wa wakimbizi kutoka Syria kwa muda mrefu."
Raia wa Syria wametafuta hifadhi nchini Uturuki, Lebanon, Jordan na Iraq tangu mwaka 2011yalipoanza maandamano ya kuipinga serikali, ambayo yaligeuka na kuwa mgogoro kati ya waasi, wapiganaji wa kundi la IS, vikosi vya serikali na vile vinavyounga mkono na mataifa ya kigeni.
Watoto 500,000 Syria hawamo shuleni
Clements alisema kando na wakimbizi hao milioni 5 waliotafuta hifadhi nje ya Syria, kuna karibu watu millioni 13.5 walioachwa bila makao ndani ya Syria, na baadhi yao wamelazimika kuhama hama sio mara mbili, bali tatu au hata nne. "Hawa ni watu ambao hawawezi kuzisaidia familia zao, wanaishi kwa hofu ya kushambuliwa kwa makombora, hawawezi kuwapeleka watoto wao shuleni," alisema Clements. Kwa mujibu wa takwimu za shirika la UNHCR, watoto millioni moja unusu ndani ya Syria hawamo shuleni.
Taifa la Kuwait ni mfadhili wa sita kwa ukubwa wa shirika la UNHCR, na kati ya mwaka 2013 na mwaka 2015 taifa hilo lilitoa msaada wa karibu dola millioni 360. Naibu kamishna huyo wa shirka la UNHCR, alisema msaada waliopokea kutoka Urusi na Uchina ni mwingi ukiliganishwa na ule wa mataifa ya Ghuba japo yanajitahidi.
Mashambulio ya kemikali yajadiliwa
Alipoulizwa iwapo wimbi la wakimbizi kutoka mataifa yanayokabiliwa na migogoro kama Syria, Iraq na Yemen linatazamiwa kupunguwa, Clements alijibu kwa ufupi kuwa ingawa matumaini ni kupatikana ufumbuzi wa kisiasa, lakini hali haionekani kuwa nzuri.
Wakati huo huo, Uingereza imejutia hatua ya kutochukua hatua mwaka 2013 kufuatia mashambulizi ya gesi nchini Syria licha ya kutishia kuwa matumizi ya silaha za kemikali ni uvukaji mpaka. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Boris Johnson, alisema hayo wakati wa mkutano wa kimataifa kuhusu Syria ulioandaliwa na Umoja wa Ulaya mjini Brussels hapo Jumatano.
Mkutano huo hata hivyo uligubikwa na mashambulizi ya silaha za kemikali katika mkoa wa Idlib nchini Syria mapema wiki hii ambalo kufikia sasa limesababisha vifo vya watu 72. Uingereza, Marekani na mataifa mengine duniani yameilaumu serikali ya Syria kwa kufanya mashambulizi hayo. Ikulu ya White House imeulaumu utawala wa awali wa Barack Obama kwa kushindwa kuichukua hatua kali serikali ya Syria ili kuzuia mashambulizi kama hayo.
Mwandishi: Jane Nyingi/RTR/dpa
Mhariri: Mohammed Khelef