1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAsia

UN yathibitisha mauaji Kabul baada ya Pakistan kushambulia

23 Februari 2026

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan (UNAMA) umesema umepokea ripoti za kuaminika za vifo vya raia wakiwemo wanawake na watoto kufuatia mashambulizi mapya ya Pakistan nchini Aghanistan.

UN | zu Verlängerung Afghanistan Mandat
UN: Yathibitisha mauaji ya raia katika shambulizi la Pakistan, Afghanistan Picha: Morteza Nikoubazl/REUTERS

UNAMA imesema mashambulizi yaliyofaynya usiku wa kuamkia leo yameyalenga maeneo manne katika mikoa ya Nangarhar na Paktika. Huko Nangarhar, tawimu za awali zinaonyesha kuwa raia 13 waliuwawa huku wengine 7 wakijeruhiwa. Idadi iliyokusanywa na mashirika ya ndani Afghanistan, yaliwekaidadi ya waliouwawa kuwa 18. Kulingana na masemaji wa polisi wa Nangarhar, miili mitano bado imekwama chini ya vifusi vya majengo yaliyoporomoka.

Kwengineko wizara ya elimu ya Afghanistan imesema wanafunzi 8 ni miongoni mwa waliouwawa. Mkoani Paktika nako shambulio moja lililenga shule na kuuharibu pia msikiti uliokuwa karibu, shambulizi jengine la angani lililenga jengo moja lililokuwa tupu. UNAMA hata hivyo imesema katika tukio hilo hakuna yeyote aliyeathiriwa kwa mashambulizi hayo.

Pakistan imesema imeshambulia maeneo ya wanamgambo nchini Afghanistan baada ya kudai kuwa wanamgambo hao wamekuwa wakitekeleza mashambulizi nchini mwake hasa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani. Pakistan imesema wanamgambo hao wanaishambulia kutoka Kabul.

UNAMA sasa imetoa wito kwa pande zote mbili Afghanistan na Pakistan kuwa wavumilivu, kuachana na vita na uhasama na kuzuwia madhara zaidi kwa raia wa pande zote.

Wizara ya Ulinzi Afghanistan yaapa kulipiza kisasi

Hapo jana Afghanistan ilimuita Balozi wa Pakistan nchini humo na kumuonya kuhusu majibu ya mashambulizi hayo huku Wizara ya ulinzi ya Afghanistan imesema inapanga shambulio la kulipiza kisasi, hali ambayo inahofiwa kuzidi kutia doa mahusiano ya mataifa hayo mawili. Mashambulizi ya Pakistan yamekosolewa vikali na wanasiasa karibu wote wa Afghanistan.

Wizara ya ulinzi ya Afghanistan imesema inapanga shambulio la kulipiza kisasi, hali ambayo inahofiwa kuzidi kutia doa mahusiano yake na Pakistan.Picha: Anton Novoderezhkin/Kommersant Photo/Sipa USA/picture alliance

Shambulizi hili limetokea siku kadhaa baada ya Afghanistan kuwaachia huru wanajeshi watatu wa Pakistan katika juhudi zilizosimamiwa  na Saudi Arabia kwa nia ya kupoza mvutano kati ya pande hizo mbili kufuatia miezi kadhaa ya makabiliano makali ya mpakani.

Pakistan inaituhumu Afghanistan kutoa hifadhi kwa makundi ya wapiganaji wanaotishia usalama wa mipaka yake madai ambayo watawala wa Taliban wamekuwa wakiyakanusha.

Mazungumzo yaliyosimamiwa na Qatar na Uturuki ya kujaribu kupunguza mvutano kati ya majirani hao wawili  yameshindwa kutuliza hali. Mataifa yote mawili yanaendelea kushutumiana kuwakinga wanamgambo wanaowashambulia katika maeneo ya mipakani.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa raia 70 wa Afghanistan waliuwawa huku 478 wakajeruhiwa katika miezi mitatu ya mwisho ya 2025 katika shambulizi linalodaiwa kufanya na Pakistan.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW