UN yautaka utawala wa kijeshi Guinea kuruhusu maandamano
30 Mei 2022Katika taarifa, msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu Seif Magango amesema wanazitaka serikali za mpito kuhakikisha kunakuwa ulinzi wa kweli wa demokrasia ikiwemo kuheshimu haki za uhuru wa kujieleza, kujumuika na mikutano ya amani.
Guinea imekuwa ikiongozwa na jeshi tangu majeshi yakiongozwa na kanali Mamady Doumbouya kumuondoa madarakani rais aliyechaguliwa Alpha Conde mwezi Septemba mwaka uliopita.
Soma pia: Guinea: Doumbouya atangaza kipindi cha mpito cha miezi 39
Jeshi hilo lilitangaza marufuku ya maandamano ya kisiasa mnamo Mei 13 baada ya kutangaza kipindi cha mpito cha miaka 3 kabla kurudishwa kwa utawala wa kiraia.
"Tunatoa wito kwa mamlaka ya mpito kuondoa marufuku walioiweka dhidi ya maandamano ya umma," alisema msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Seif Magango katika taarifa.
"Tunauhimiza utawala wa mpito kuhakikisha ulinzi wa kweli na wa maana wa demokrasia - ikiwemo kuheshimu haki ya kujieleza, kujumuika na kukusanyika kwa amani," aliongeza.
Hatua za utawala wa kijeshi 'zinakiuka utaratibu na viwango vya kimataifa kuhusu haki za binadamu na ni pigo katika njia ya kuimarisha demokrasia na utawala wa sheria," alisema.
Soma pia: Watawala wapya Guinea watafuta kujiimarisha madarakani
Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi kuhusu hatua hizo, ikiwemo "uvunjaji wa majengo binafsi" katika mji mkuu Conakry, Siguiri katika eneo la kaskazini-mashariki na Nzerekore upande wa kusini-mashariki.
Mchakato huo uliripotiwa kulenga "kurejesha ardhi ya umma" lakini ulitokea katika wakati ambapo rufaa zilikuwa zinasubiri kusikilizwa na mahakama," Magango alisema.
Mapendekezo ya utawala wa kijeshi wa kipindi cha mpito yanapuuza matakwa ya washirika wa kikanda katika jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS), ambayo yanatoa wito wa kuwepo na ratiba ya haraka ya uchaguzi.
Kanda hiyo ya Afrika Magharibi imesimamisha uanachama wa Guinea baada ya mapinduzi.
Chanzo: AFP