1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

U.N yawatuhumu wanajeshi wa Burundi

15 Juni 2017

Ripoti iliyotolewa na wachunguzi wa Umoja wa Mataifa leo imesema wanajeshi wa Burundi pamoja na wapiganaji washirika bado wanawateka nyara, kuwatesa na kuwaua raia bila ya kujali sheria. Madai yaliyokanushwa na Burundi. 

Burundi 2 Jahre Krise - Reportage im Protestviertel Nyakabiga
Picha: DW/A. Niragira

 

Wachunguzi hao wamesema, Burundi ambayo ni mwanachama wa Baraza la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa imekataa kujibu barua alizoandikiwa waziri wa masuala ya kigeni, na kwa maana hiyo haina taarifa zozote ambazo ingefaa kuwa nazo juu ya taifa hilo la Afrika ya Kati ambako matukio ya ukiukwaji wa haki za binaadamu huwasilishwa mahakamani mara chache.

Balozi wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi Renovat Tabu amesema madai hayo yaliegemea upande mmoja na kwamba wachunguzi hao walipuuza hatua za serikali za kurejesha amani na usalama.

Burundi iliingia katika machafuko mwezi Aprili 2015, wakati rais Pierre Nkrunziza alipotangaza kugombea awamu ya tatu, hatua ambayo upinzani ulisema ilikuwa kinyume na katiba na ilikiuka makubaliano ya amani yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2005. Nkrunziza alichaguliwa kwa mara nyingine, hatua iliyoibua machafuko dhidi ya hatua yake hiyo kutoka kwa wapinzani wake.

Zaidi ya raia 700 waliuawa tangu wakati huo, huku kiasi ya watu 400,000 wakikimbilia nchi jirani, hii ikiwa ni kulingana na tume ya serikali ya masuala ya haki za binaadamu.

Tume hiyo ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa, iliyoundwa na baraza mwezi Septemba mwaka jana, imekusanya shuhuda 470 zinazohusiana na vitendo vya ukiukwaji vilivyotendwa tangu mwaka 2015, vinavyoakisi kuongezeka kwa hofu miongoni mwa raia wanaoishi uhamishoni, amesema mwenyekiti wa tume hiyo Fatsah Ouguergouz.

Zaidi ya raia 700 wameyakimbia makazi yaoPicha: S. Aglietti/AFP/Getty Images

Waathiriwa wasimulia mateso tofauti waliyopewa na wanajeshi.

Baadhi ya waathiriwa, hususan wanachama wa vyama vya upinzani ama watu walituhumiwa kuunga mkono upinzani ama kuwa wanachama wa makundi ya wapiganaji ama wanaomiliki silaha waliowaelezea mateso na hasa unyanyasaji wa kinyama uliofanywa na idara ya ujasusi ya kitaifa na polisi, mara nyingine wakisaidiwa na kundi la wapiganaji vijana linalounga mkono serikali la Imbonerakure.

"Tulikusanya ushahidi kadhaa uliodai matumizi ya virungu, vitako vya bunduki, minyororo na nyanya za umeme wakati wakiteswa. Baadhi yao walivunjika mifupa na wengine wakapoteza fahamu. Na pia walichomwa sindano ambazo haikutambulika zilikuwa na kemikali ya aina gani, wakati mwingine zilikwama kwenye miili ya waathirika hao, kunyofolewa kucha, kuunguzwa na moto na mateso mengine mengi kufanywa kwenye sehemu za siri za wanaume" amesema Ouguergouz 

Unyanyasaji huo ulifanywa zaidi kwa usiri lakini kwa ukatili, tangu mwishoni mwa mwaka 2016.

Baada ya kupotea, miili inapatikana kwenye mito, ambayo hukutwa imefungwa mikono nyuma na mara nyingine ilizamishwa na kufungwa na mawe.

John Fisher kutoka shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch amesema kwamba Burundi inalidharau baraza la Umoja wa Mataifa. Amesema mfumo wa haki wa taifa hilo unaingiliwa sana na chama tawala na haujaweza kutenda haki ya kweli kwa matukio hayo ya uhalifu.

Ameongeza kwamba upuuzwaji huu wa sheria unatuma ujumbe kwa Imbonerakure, kwamba wanajua wanaweza kuua, kubaka na kuwatisha raia na bila kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mwandishi: Lilian Mtono/reuters

Mhariri:Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW