1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yazishutumu kampuni 158 kwa uhalifu Palestina

26 Septemba 2025

Zaidi ya kampuni 150 za ndani na nje ya Israel zimeshutumiwa na Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa kwa kuhusika na kile unachosema Umoja huo kuwa ni uhalifu dhidi ya ubinaadamu ndani ya Palestina.

Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa, Volker Türk
Mkuu wa Kamisheni wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa, Volk Turk, amezikosowa kampuni zinazofaidika na uhalifu wa kivita kwenye ardhi za Palestina.Picha: Uncredited/AP/dpa/picture alliance

Umoja wa Mataifa ulitangaza siku ya Ijumaa (Septemba 26) orodha ya kampuni 158 kutoka mataifa 11 ambazo zimekuwa zikiendesha shughuli zao ndani ya ardhi za Wapalestina wakati huu mashambulizi ya Israel yakiendelea Gaza  na Ukingo wa Magharibi.

Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Umoja huo, Volker Turk, alilaani kile alichosema ni "uhalifu wa kivita Gaza na sera ya makaazi ya walowezi wa Kiyahudi kwenye Ukingo wa Magharibi" unaokaliwa kimabavu na Israel.

Kampuni kubwa kama vile Airbnb, Booking.com, Motorola Solutions na Trip Advisor ziliendelea kusalia kwenye orodha hiyo, huku kampuni nyengine kama vile Alstom na Opodo zikiondolewa.

Nyingi ya kampuni hizo zina makao yake ndani ya Israel, lakini pia ziko zenye makao yake mkuu nchini Kanada, China, Ufaransa, Ujerumani, Luxembourg, Uholanzi, Ureno, Uhispania, Uingereza na Marekani.

Ripoti hiyo ya  Umoja wa Mataifa iliyotolewa mjini Geneva ilizitaka kampuni hizo "kuchukuwa hatua muafaka kushughulikia athari za ushiriki wao kwenye uvunjaji wa haki za binaadamu, ikiwemo kulipa fidia na kutoa ushirikiano kwenye uchunguzi" dhidi yao. 

Watu 22 wauawa Ukanda wa Gaza

Idara inayohusika na ulinzi wa raia kwenye Ukanda wa Gaza ilisema kuwa watu 22 waliuawa siku ya Ijumaa, wakiwemo 11 kwenye Jiji la Gaza, huku taarifa ya jeshi la Israel ikisema kuwa kikosi chake cha anga kimeshambulia maeneo zaidi ya 140 kwenye Ukanda huo. 

Majengo kwenye Jiji la Gaza yakiwa yamefudikizwa kwa mashambulizi makali ya jeshi la Israel.Picha: Eyad Baba/AFP

Picha ya video kutoka shirika la habari la AP inaonesha majengo yaliyoharibiwa vibaya kwenye kambi ya wakimbizi ya Al-Shati karibu na Jiji la Gaza.

Kwenye mkanda huo, majengo yanaonekana yakiwa yamebiruliwa juu chini-chini juu, huku watu, akiwemo msichana asiyekuwa na viatu, wakisaka manusura na mali zao kwenye vifusi vya majengo hayo.

Akizungumza akiwa kwenye mojawapo ya majengo yaliyoporomoshwa  mchana wa Ijumaa, Abdallah Majdalawi, ambaye ni mfanyakazi wa Idara ya Ulinzi wa Raia, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba kinachoshuhudiwa kwenye Jiji la Gaza ni mauti na uharibifu tu.

"Uharibifu huu unaendelea kwa majengo mengi ya raia. Hadi muda huu, wafanyakazi wa ulinzi wa raia wanaendelea kuwaokowa manusura. Hadi hapa, shahidi mmoja na majeruhi watatu wamepatikana kwenye jengo hili. Bado tunaendelea kuwatafuta waliopotea na majeruhi walio chini ya jengo hili." Alisema mfanyakazi huyo.

Takribani miaka miwili tangu tukio la Oktoba 7, 2023 pale wanamgambo wa Kipalestina walipolivamia eneo la kusini mwa Israel na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 1,200 na kuwachukuwa wengine mateka zaidi ya 200, hatua za ulipizaji kisasi za Israel zimeangamiza maisha ya Wapalestina 65,549, kwa mujibu wa rikodi zinazotambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW