1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfghanistan

Zaidi ya raia 1000 wauawa katika mashambulizi Afghanistan

27 Juni 2023

UN yasema imeorodhesha idadi kubwa ya raia waliouawa na kujeruhiwa nchini Afghanistan tangu Taliban ilipoingia madarakani, licha ya kupungua kwa kiasi kikubwa cha majeruhi ikilinganishwa na miaka ya nyuma ya vita na uasi

Afghanistan | Taliban Kämpfer in der Nähe von Kabul im Jahr 1996
Picha: Hurriyet/AP/picture alliance

Kulingana na ripoti mpya ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan UNAMA, tangu kundi la Taliban lilipoingia madarakani katikati ya Agosti 2021 hadi mwisho wa Mei, kulikuwa na wahanga 3,774 wa kiraia, wakiwemo 1,095 waliouawa katika vurugu nchini humo. Idadi hiyo inalinganishwa na wahanga 8,820  wa kiraia, wakiwemo 3,035 waliouawa katika mwaka 2020 pekee. Kulingana na ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa, robo tatu ya mashambulizi hayo tangu Taliban kuingia madarakani,  yalitekelezwa kwa kutumia vifaa vya milipuko vilivyotengenezwa kienyeji katika maeneo yenye watu wengi, yakiwemo maeneo ya ibada, shule na masoko. Miongoni mwa waliouawa ni wanawake 92 na watoto 287.

Takwimu zaonesha ongezeko la madhara yanayotokana na mashamabulizi

Takwimu hizo zinaonyesha ongezeko kubwa la madhara kwa raia yanayotokana na mashambulizi ya vilipuzi kwenye maeneo ya ibada - mengi yakiwa ya jamii ya Waislamu wachache wa madhehebu ya Kishia, ikilinganishwa na kipindi cha miaka mitatu kabla ya kuingia madarakani kwa Taliban. Taarifa hiyo pia ilisema kuwa watu wasiopungua 95 waliuawa katika mashambulizi dhidi ya shule , taasisi za elimu na maeneo mengine ambayo yalilelenga zaidi jamii ya Kishia ya Hazara. Taarifa hiyo imesema mashambulizi mengi yalifanywa na tawi la kundi linalojiita dola la kiislamu IS, linalojulikana kama dola la kiislamu katika jimbo la Khorasan, kundi la wanamgambo wa Kisunni ambalo ni mpinzani mkuu wa Taliban.

Uongozi wa Taliban wahimizwa kulinga maisha ya Waafghanistan

Roza Otunbayeva - Mkuu wa UNAMAPicha: Shen Hong/Xinhua/IMAGO

Fiona Frazer, mkuu wa huduma ya haki za binadamu katika ujumbe huo wa UNAMA, amesema mashambulizi hayo dhidi ya raia na mali zao hayafai na yanapaswa kukomeshwa mara moja. Pia aliuhimiza uongozi wa Taliban kuzingatia wajibu wao wa kulinda haki ya maisha ya watu wa Afghanistan. Hata hivyo, ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema idadi kubwa ya vifo hivyo ilitokana na mashambulizi ambayo hakuna aliyedai kuhusika nayo ama ambayo ujumbe wa Umoja wa Mataifa haukuweza kuhusisha na kundi lolote. Ripoti hiyo haikutoa idadi ya vifo hivyo. Ripoti hiyo pia ilielezea wasiwasi kuhusu hatari ya mashambulizi ya kujitoa mhanga tangu Taliban ilipochukuwa uongozi huku mashambulizi machache yakisababisha vifo zaidi  vya raia.

Uongozi wa taliban wasema nchi hiyo imeimarika kwa hatua

Katika kujibu, wizara ya mambo ya nje ya Afghanistan inayoongozwa na Taliban, imesema kwamba hali nchini humo imeimarika kwa hatua tangu Agosti mwaka 2021. Taliban pia imesema kuwa usalama umehakikishwa kote nchini humo na kuongeza kuwa uongozi wake unazingatia usalama wa maeneo ya ibada na madhabahu matakatifu yanayojumuisha maeneo ya Kishia kuwa suala la kipaumbele.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW