UN: Wafanyakazi 1,000 wa misaada waliuawa tangu 2023
9 Aprili 2026
Akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York, Mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, amesema jumla ya wafanyakazi 1,010 wameuawa katika nchi 21 kati ya mwaka 2023 hadi 2025, huku karibu nusu ya vifo hivyo vikitokea Gaza wakati wa vita kati ya Israel na Hamas. Aliongeza kuwa wengi wao waliuawa wakiwa kazini, wakigawa chakula na misaada au wakiwa katika misafara iliyoratibiwa rasmi.
Takwimu zinaonesha kuwa maeneo yaliyoathirika zaidi na mashambulizi makubwa ni maeneo ya Palestina, yakifuatiwa na Sudan, Sudan Kusini, Ukraine na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Katika mwaka 2025 pekee, wafanyakazi 326 waliuawa, huku mwaka 2024 ukiweka rekodi ya juu zaidi ya vifo 383.
Fletcher amesema hali hiyo si ajali bali ni matokeo ya kupuuzwa kwa sheria za kimataifa, akieleza kuwa baadhi ya mashambulizi yalifanywa hata na mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa, jambo linalozua wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa wahudumu wa misaada duniani.
"Watoa misaada wanajua tunakabiliwa na hatari; hiyo ndiyo asili ya kazi yetu na maeneo tunayofanyia kazi. Vifo hivi havitokani na sisi kutojali maisha yetu, bali vinatokana na pande zinazohusika katika migogoro kutojali maisha yetu."
Wahusika wa mauaji hawawajibishwi
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na usalama, Gilles Michaud, amesema wahusika wa mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa misaada mara chache huwajibishwa, huku mifumo ya kulinda wahudumu hao ikiendelea kudhoofika.
Ameongeza kuwa changamoto kama kucheleweshwa kwa visa, kunyimwa vifaa muhimu vya usalama na kupuuzwa kwa taratibu za usalama zimeongeza hatari kwa wafanyakazi wa misaada, hasa katika maeneo yenye migogoro mikubwa.
"Mbinu za jadi za kushirikiana na wahusika wa migogoro ili kulinda wafanyakazi wa misaada na mali zao, ambazo hapo awali zilikuwa za kawaida na zenye ufanisi, sasa mara nyingi zinapingwa au kukwamishwa. Bila ushirikiano madhubuti na uungwaji mkono kutoka kwa serikali za kitaifa, hatari huongezeka na wenzetu hupoteza maisha."
Naye Mwakilishi wa Kudumu na Mkuu wa Ujumbe wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu katika Umoja wa Mataifa, Elyse Nicole Mosquini, ameonya kuwa dunia inapoteza ubinadamu katika vita, akitaka uwajibikaji kwa wale wanaoshambulia wahudumu wa misaada.
"Waheshimiwa, hali hii haiwezi kuendelea. Pande zinazohusika katika migogoro ya silaha haziwezi kuendelea kupigana vita bila mipaka. Hili ni jukumu la kisheria, kimaadili na kibinadamu. Watu wanaowasaidia wengine katika vita na majanga ya kibinadamu hawapaswi kuuawa. Hawapaswi kulengwa."
Fletcher ameyataka mataifa 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa kutekeleza matakwa ya azimio la mwaka 2024 kwa kuwalinda wafanyakazi wa misaada na kuhakikisha uwajibikaji kwa uhalifu unaofanywa dhidi yao.