1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaItaly

UN: Zaidi ya wahamiaji 180,000 wameingia Ulaya mwaka 2023

29 Septemba 2023

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema takriban watu 186,000 wamewasili Ulaya kupitia bahari ya Mediterania mwaka huu.

Kundi la wahamiaji wakiwasili katika eneo la Dover, Kent nchini Uingereza
Kundi la wahamiaji wakiwasili katika eneo la Dover, Kent nchini UingerezaPicha: Gareth Fuller/empics/picture alliance

Mkurugenzi wa ofisi ya UNHCR mjini New York Ruven Menikdiwela ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba watu 130,000 wamesajili nchini Italiaidadi hiyo ikiwa ni ongezeko la asilimia 83 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Menikdiwela ameeleza kuwa, zaidi ya watu 2,500 hawajulikani waliko au wamekufa tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi Septemba 24.

Hivi karibuni, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM lilitoa takwimu zilizoonyesha kuwa, zaidi ya watu 2,700 hawajulikani waliko au wamekufa.

Ongezeko la idadi ya wahamiaji tayari limesababisha mivutano ndani ya Umoja wa Ulaya juu ya hatua za kudhibiti wimbi la wahamiaji.

Viongozi wa Mediterania wakutana kujadili juu ya suala la wahamiaji

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (kushoto) Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni (katikati) na Rais wa bunge la Ulaya Roberta Metsola (kulia) katika mkutano mjini BrusselsPicha: Dursun Aydemir/AA/picture alliance

Viongozi wa nchi tisa za Mediterania na kusini mwa Ulaya, akiwemo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni, wanakutana leo nchini Malta kwa mazungumzo yatakayojikita juu ya suala la wahamiaji.

Mkutano huo unafanyika siku moja tu baada ya shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia wakimbizi la UNHCR kusema kwamba zaidi ya wahamiaji 2,500 wamepoteza maisha au hawajulikani waliko wakati walipokuwa wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterania mwaka huu - idadi hiyo ikiwa juu zaidi ikilinganishwa na kipindi sawa na hicho mwaka 2022.

Mkutano huo wa Malta unajiri pia wakati mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya wanakaribia kuafikiana juu ya pendekezo la sheria mpya ya jinsi Umoja huo utakavyoshughulikia suala la waomba hifadhi na wahamiaji, huku makubaliano juu ya hilo yakitarajiwa kufikiwa katika siku zijazo.

Soma pia: Italia yapitisha kanuni mpya kuwakabili wahamiaji

Kumekuwepo na msukumo mpya wa kufikia makubaliano juu ya pendekezo la sheria hizo mpya hasa kufuatia ongezeko la wahamiaji katika kisiwa kidogo cha Italia cha Lampedusa mapema mwezi huu.

Serikali ya Meloni inayoegemea siasa za mrengo mkali wa kulia, iliyochaguliwa kutokana na sera yake ya kupinga wahamiaji, imevutana na Ujerumani na Ufaransa huku Meloni akishinikiza nchi nyengine za Umoja wa Ulaya kugawanya mzigo wa kuwahudumia wahamiaji.

Hadi kufikia sasa, idadi ya wahamiaji waliowasili katika kisiwa cha Lampedusa imepindukia 133,000.
 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW