UN: Zaidi ya watu 300 wameuawa Ethiopia tangu Novemba
8 Machi 2022Michelle Bachelet, ambaye ni mkuu wa shirika la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa akiwa mjini Geneva ameliambia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja huo, kwamba hali ya haki za binadamu pamoja na hali ya usalama nchini Ethiopia, zimeendelea kudorora zaidi tangu mwisho wa mwezi Novemba.
Kwa mujibu wa Bachelet, ofisi yake imeendelea kupokea ripoti ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika majimbo ya Afar, Amhara na Tigray.
Wahanga wa Tigray wafungua kesi dhidi ya Ethiopia
Ofisi yake ilirekodi visa 304 vya mauaji na majeruhi 373 kufuatia mashambulizi ya ndege. Ripoti yake ilijumuisha matukio ya kati ya Novemba 22 hadi Februari 28 mwaka huu.
Alielezea wasiwasi mkubwa uliopo kuhusu mashambulizi ya angani yanayofanywa na vikosi vya serikali ya shirikisho la Ethiopia na vilevile vikosi vya Tigray hususan katika jimbo la Tigray na pia Afar.
Ethiopia: Wapiganaji wa Tigray walaumiwa kwa ubakaji
"Katika kipindi hicho, ofisi yetu imepokea visa 306 vya ubakaji vilivyofanywa na vikosi vya Tigray katika jimbo la Amhara kati ya Novemba mosi hadi Disemba 5 mwaka 2021. Visa vingi vya manusura wa madhila hayo ni wanawake, idadi ndogo ikiwa ni wanaume. Manusura wengi hawajapokea msaada wa aina yoyote kufuatia dhuluma dhidi yao," amesema Bachelet.
Bachelet alisisitiza kuwa mashambulizi dhidi ya raia na mali yao yalifanywa na pande husika kwenye machafuko hayo.
Ethiopia yaondoa hali ya hatari mapema, ikisema vita vimetulia
Ameshutumu uharibifu mkubwa wa shule na vituo vya afya katika jimbo la Amhara na Afar kufuatia mashambulizi ya vikosi vya serikali dhidi ya vikosi vya Tigray.
Amesema mnamo Januari 24, vikosi vya Tigray vilitumia zana nzito za kivita kushambulia maeneo kadhaa ya Afar na kuwa duru za kuaminika zimeeleza raia kadhaa waliuawa.
Alilaani matukio mengine ya ukiukwaji wa haki za binadamu yaliyofanywa kwenye machafuko hayo yaliyoanza Novemba 2020, wakati Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abiy Ahmed, alipovituma vikosi vyake katika jimbo la Tigray, kufuatia madai kwamba chama tawala katika jimbo hilo TPLF, kilikuwa kikipanga kushambulia kambi za jeshi lake.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, vita hivyo vya Ethiopia vimesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwaweka mamia ya maelfu katikahatari ya njaa.
Bachelet amesema mashambulizi na machafuko yanayoshuhudiwa Ethiopia yanaibua wasiwasi kwa msingi wa sheria ya kimataifa ya kiutu, inayopiga marufuku mashambulizi ya makusudi dhidi ya raia na maeneo yao.
(AFPE, RTRE)