UN: Zaidi ya watu milioni 7 wamekimbia mapigano Sudan
22 Desemba 2023Kwa mujibu wa shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM, hadi watu 300,000 wamehama kutoka mji wa Wad Madani katika jimbo la Al-Jazira, katika wimbi jipya la uhamaji wa watu wengi.
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, amesema watu wengine milioni 1.5 wamekimbilia katika mataifa jirani, na kuongeza kuwa uhamaji huu mpya utafikisha idadi ya watu waliotoroka makazi yao nchini Sudan kuwa milioni 7.1, na kuufanya huu kuwa mzozo mkubwa zaidi wa wakimbizi duniani.
Soma pia: WFP yasimaisha mpango wa msaada wa chakula kwa muda katika baadhi ya maeneo ya jimbo la Gezira
Watu zaidi ya nusu milioni wamepata hifadhi katika jimbo la Al-Jazira, ambalo lilikuwa linazalisha chakula kwa wingi kabla ya vita.
Shirika la kimataifa la Kamati ya Msalaba Mwekundu, ICRC, lililoondoa wafanyakazi wake wiki iliyopita baada ya mapigano kufika katika mji wa Wad Madani, limetoa wito wa kuwezesha kufika kwa mahitaji ya kuokoa maisha katika maeneo yote yalioathiriwa na mapigano wakati ambapo mahitaji ya kibinamu yanaongezeka.
Hofu ya kukosekana kwa msaada ya kiutu
Kati ya watu milioni 25 wenye uhitaji nchini Sudan, Umoja wa Mataifa umeweza kuwafikia watu milioni nne tu, na hata msaada kwa watu hao unaweza kusimama muda wowote, alisema Clementine Knweta-Salami katika mahojiano na shirika la habari la Ufaransa, AFP, ikiwa ukosefu sugu wa ufadhili utaendelea.
Mratibu huyo wa masuala ya kiutu kwa ajili ya Sudan, alisema miezi minane tangu kuzuka kwa vita kati ya majenerali wawili hasimu, hali nchini Sudan imegeuka kuwa janga. Baadhi ya wafanyakazi wa msaada wameutaja mzozo huo kuwa vita vilivyosahaulika.
Soma pia: RSF yachukua udhibiti wa mji wa Wad Madani
Aprili 15, mkuu wa mejeshi Abdel Fattah al-Burhan na naibu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo, anaeongoza kundi la RSF, waligeuziana silaha, miaka miwili baada ya washirika hao wa zamani kupanga kwa pamoja mapinduzi ya mwaka 2021 yalioundoa mamlakani utawala wa kiraia.
Vikosi vyao vimeua zaidi ya watu 12,190 katika mapambano yao ya kuwania madaraka, kulingana na mradi wa ufuatiliaji wa mizozo ya sihala, ACLED.
Mapema wiki hii vikosi vya jeshi vilitangaza kujiondoa mji wa Wad Madani, baada ya RSF kutangaza kuutwa mji huo.
Akizungumza na maafisa wa eneo la kijeshi la Bahari ya Shamu katika mji wa Port Sudan jsiku ya Alhamisi, Jenerali Burhan alisema atawajibisha makanda wazembe waliohusika na kujiondoa huko, yakiwa matamshi ya wazi ya Burhan kuhusiana na kunaguka kwa mji wa Wad Madani.