UN: Zaidi ya watu milioni moja wamekimbia makwao Myanmar
3 Juni 2022Zaidi ya nusu ya idadi hiyo waliyakimbia makaazi yao baada ya jeshi kuchukua madaraka mwaka uliopita.
Shirika hilo la kiutu limesema kwenye ripoti yake kwamba hali inazidi kuwa tete kufuatia machafuko yanayoendelea kati ya utawala wa kijeshi na wapinzani wao.
Suu Kyi ahukumiwa miaka 5 jela kwa ufisadi
Bei ya bidhaa muhimu inazidi kupanda na ufadhili kwa waathiriwa hautoshi. Ripoti hiyo imeangazia hali ilivyo katika kipindi cha nyuma hadi Mei 26.
Kulingana na ripoti hiyo, jeshi limekuwa kisiki na inazuia uwezekano wa misaada ya kiutu kupelekwa kwa waathiriwa hasa maeneo yaliyomo chini ya udhibiti wake, hivyo kutatiza shughuli za kiutu.
Maafisa wa jeshi na polisi walipoanza kutumia nguvu nyingi dhidi ya waandamanaji, maandamano yaligeuka kuwa ya vurugu. Taifa hilo likatumbukia katika kile wataalamu wa Umoja wa Mataifa walikitaja kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Marekani yasema jeshi la Myanmar limefanya mauaji ya halaiki
Shirika la OCHA limesema mapigano yameendelea kuongezeka katika siku za hivi karibuni.
"Athari dhidi ya raia zinazidi kuwa mbaya kufuatia mashambulizi ya kikatili ya mara kwa mara na matumizi ya vilipuzi hatari,” ripoti imeeleza.
Imesema zaidi ya watu 694,300 wameyakimbia makwao tangu jeshi lilipochukua usukani. Maelfu wengine wanalazimika kukimbia kwa mara ya pili au tatu, na takriban watu 346,000 hususan jamii za walio wachache, walikadiriwa kuyakimbia makaazi yao kabla ya jeshi lilipofanya mapinduzi.
Mwaka mmoja wa mapinduzi ya kijeshi Myanmar waadhimishwa kwa maandamano
Ripoti hiyo imesema takriban watu 40,200 wamekimbilia mataifa Jirani na zaidi ya majengo 12,700 zikiwemo nyumba, makanisa na shule zimeharibiwa.
Kulingana na OCHA, hadi mwisho wa robo ya mwaka huu, watu milioni 2.6 walikuwa wamepata misaada ya kiutu Myanmar. Idadi jumla ya nchi hiyo ni watu zaidi ya milioni 55.
Imetahadharisha kwamba ni asilimia 10 pekee ya ufadhili wa kiutu mwaka huu nchini Myanmar imeshafanikishwa, hivyo kuna upungufu wa dola milioni 740.
Mwezi uliopita, mkuu wa shirika linalowashughulikia wakimbizi katika Umoja wa Mataifa Filippo Grandi alisema idadi ya watu ulimwenguni kote wanaolazimika kuyakimbia makwao kufuatia machafuko, ukiukaji wa haki za binadamu, mateso na mauaji imepindukia watu milioni 100, hiyo ikiwa mara ya kwanza kulingana na rekodi zao.
Hadi mwisho wa mwaka uliopita, machafuko na mizozo katika baadhi ya nchi ikiwemo Ethiopia, Burkina Faso, Myanmar, Nigeria, Afghanistan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilisababisha takriban watu milioni 90 kuwa wakimbizi.
Vita nchini Ukraine vimefanya idadi hiyo kupindukia milioni 100.
(AFPE)