1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaLebanon

Unachohitaji kufahamu kuhusu kundi la Hezbollah

5 Januari 2024

Hezbollah imekita mizizi nchini Lebanon ambakoimejiimarisha kisiasa na kijeshi. Jukumu lake katika mzozo wa sasa kati ya Israel na Hamas huko Gaza linaweza kuongezeka baada ya kifo cha afisa wa ngazi ya juu wa Hamas.

Libanon Beirut | Rede Hisbollah-Führer | Sayyed Hassan Nasrallah
Watu wakiangalia kwenye runinga hotuba ya Kiongozi wa kundi la Hezbollah Hassan Nasrallah aliyoitoa 03/01/2024, katika siku ya kumuenzi Jenerali mashuhuru wa Iran Qasem Soleimani alieuawa kwa shambulizi la droni la Marekani mwaka 2020.Picha: ANWAR AMRO/AFP

Saleh al-Arouri alikuwa naibu kiongozi wa kundi la Hamas na aliuawa kwa shambulio la ndege isiyo na rubani mjini Beirut siku ya Jumanne. Al-Arouri alikuwa afisa muhimu wa Hamas na hata Hezbollah, makundi mawili yanayoungwa mkono na Iran na ambayo yameorodheshwa na Israel, Marekani, Ujerumani na mataifa mengine kadhaa ya Magharibi kuwa  makundi ya kigaidi.

Ingawa hakuna aliyedai kuhusika na shambulio hilo, ambalo pia liliwaua maafisa wengine kadhaa wa Hamas, Waziri Mkuu wa Lebanon, Najib Mikati, amelitaja shambulio hilo kuwa ni "uhalifu mpya wa Israeli unaolenga kuitumbukiza Lebanon katika hatua mpya ya makabiliano." Israel hadi sasa haijazungumzia chochote juu ya tukio hilo, lakini Mark Regev, mshauri wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, amesema kuwa yeyote aliyefanya shambulio hilo hakuilenga Lebanon wala Hezbollah, bali Hamas.

Soma pia: Hezbollah wadai kudungua droni ya Israel karibu na Lebanon

Kifo cha al- Arouri kinaweza kuwa kilichovuka mpaka kwa Hezbollah ambapo kiongozi wa kundi hilo la Waislamu wa madhehebu ya Shia, Hassan Nasrallah, ameapa mara kwa mara kuwa angeishambulia Israel iwapo jeshi la nchi hiyo litawalenga maafisa wa Palestina nchini Lebanon. Jambo linaloibua wasiwasi wa mzozo huo kutanuka katika maeneo mengine ya Mashariki ya Kati.

Je, unaifahamu Hezbollah?

Saleh al-Arouri Naibu Kiongozi wa Kundi la Hamas ziarani mjini Damascus nchini Syria: 21.12.2010 katika mkutano wa kupinga kamatakamata la kisiasa katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.Picha: APA Images/ picture alliance

Hezbollah ni kundi linalofadhiliwa na Iran lenye makao yake nchini Lebanon ambako pia lilianzishwa. Jina lake linamaanisha "Chama cha Mungu". Tawi lake la kijeshi lililitajwa mwaka 2022 na kituo cha Wilson cha Marekani kuwa ni imara na kitisho kikubwa katika Mashariki ya Kati na hata ulimwenguni.

Kiongozi wa kundi hilo ni Hassan Nasrallah, ambaye amekuwa akijigamba kuwa Hezbollah ina wapiganaji karibu 100,000. Walakini, makadirio mengine ya wataalam yanaonyesha kuwa idadi hiyo inaweza kuwa chini ya hapo.

Soma pia: Mauaji ya kiongozi wa Hamas Beirut yazidisha hatari ya kusambaa kwa vita vya Gaza

Mbali na harakati za kijeshi, Hezbollah inajihusisha pia katika shughuli za kisiasa na kijamii nchini Lebanon. Kutokana na kwamba theluthi moja ya Walebanon ni kutoka madhehebu ya Shia, asilimia 89 ya watu walikuwa na maoni chanya juu ya Hezbollah katika matokeo ya kura ya maoni ya mwaka 2020. Hata hivyo, Walebanon wengine wanalipinga kundi hilo, wakisema linaielekeza nchi yao katika hali ya migogoro.

Je, Hezbollah iliundwa vipi?

Mfuasi wa kundi la Hezbollah akionyesha picha ya naibu kiongozi wa kundi la Hashd al-Shaabi la Iraq, Abu Mahdi al-Mohandes (kushoto), naibu kiongozi wa kundi la Hamas Saleh al-Arouri (katikati) na Jenerali mashuhuri wa Iran Qasem Soleimani wote wakiwa waliuawa.-Maandishi kwenye picha: "Damu ni moja, Adui ni mmoja na pambano ni moja."Picha: Marwan Naamnai/dpa/picture alliance

Kundi la Hezbollah lilianzishwa mwaka 1982 wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Lebanon vilivyodumu kwa miaka 15. Mzozo huo ulioanza mwaka 1975, ulisababisha jamii mbalimbali za Lebanon wakiwemo Waislamu, Wakristo, watu wa mrengo wa kushoto na wazalendo wa Kiarabu kuzozana. Syria na makundi yenye silaha ya Wapalestina yalihusika pia wakati huo.

Wakati Walebanon wakikabiliana wenyewe kwa wenyewe, vikosi vya Israel vilivamia kusini mwa Lebanon mnamo 1978 na mwaka 1982 ili kuwafurusha wapiganaji wa Palestina waliokuwa wakilitumia eneo hilo kama kituo cha kupanga mikakati ya kuishambulia Israel.

Soma pia: Marekani yashambulia wanamgambo wanaoiunga mkono Iran

Baadaye, kundi la Waislamu wa madhehebu ya Shia waliamua kupambana na majeshi ya Israel. Nayo Iran kwa kuzingatia fursa ya kujijengea ushawishi katika ulimwengu wa Kiarabu, ilianza kutoa mafunzo na kuwafadhili wanamgambo hao wapya.

Iran imekuwa ikifadhili makundi kadhaa huko Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na Hamas, Hezbollah na makundi mengine ya wanamgambo nchini Iraq. Hivi karibuni, serikali ya Marekani ilikadiria kuwa Iran inatoa ufadhili wa kiasi cha dola milioni 700 kila mwaka kwa kundi la Hezbollah.

Ni zipi sera za Hezbollah?

Kombora lililotengenezwa nchini Iran likionyeshwa mbele ya picha ya kiongozi wa Hezbollah ya Lebanon Sayyed Hassan Nasrallah wakati wa maandamano ya kikosi cha wanamgambo wa Basij cha Iran kuwaunga mkono Wapalestina. Tehran, Iran:24.11.2023Picha: Vahid Salemi/AP Photo/picture alliance

Mnamo mwaka 1985, Hezbollah ilitoa ilani ambayo iliorodhesha idadi ya malengo yake ikiwa ni pamoja na kuyaondoa mataifa ya kikoloni ya Magharibi nchini Lebanon, kuisambaratisha dola ya Israel na utiifu kwa Iran. Sehemu ya sera ya awali ya Hezbollah ilikuwa ikitoa pia wito wa kuwepo utawala wa Kiislamu nchini Lebanon kwa kuzingatia mtindo wa kidini wa Iran.

Lakini, baada ya muda kadhaa,  malengo ya ndani ya Hezbollah  kwa kiasi fulani yalipunguza makali kwani kundi hilo lilianza kujihusisha zaidi na harakati za kisiasa. Mnamo mwaka wa 2009, Hezbollah ilichapisha ilani mpya iliyokiri kwamba uwepo wa serikali ya Kiislamu haufai kwa nchi ya Lebanon.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW