1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Mamlaka za Lebanon zilijua hatari ya kuhifadhi kemikali

Sylvia Mwehozi
3 Agosti 2021

Shirika la Human Rights Watch limesema kuwa maafisa waandamizi wa Lebanon walifahamu kitisho kilichokuwepo kutokana na kuhifadhiwa kemikali kwa miaka mingi katika bandari ya Beirut na hawakufanya chochote kuulinda umma.

Libanon | Gewaltige Explosion in Beirut
Picha: Getty Images/AFP/STR

Shirika la kimataifa la haki za binadamu la Human Rights Watch limesema kuwa maafisa waandamizi wa Lebanon walifahamu kitisho kilichokuwepo kutokana na kuhifadhiwa kemikali kwa miaka mingi katika bandari ya Beirut na hawakufanya chochote kuulinda umma.

Katika ripoti juu ya mripuko mkubwa uliotokea mwaka uliopita, Human Rights Watch imesema maafisa wale wale sasa wanajaribu kuzuia uchunguzi. Shirika hilo limetaka maafisa hao wanaohusishwa na mkasa wa mwaka jana kuwekewa vikwazo na pia kufanyike uchunguzi wa kimataifa.

Ripoti hiyo inatolewa wakati Lebanon ikifikisha mwaka mmoja tangu kutokee mkasa huo mnamo Agosti 4,wakati mripuko mkubwa ulipoutikisa mji wa Beirut  na kuwaua watu 214 huku zaidi ya wengine 6,000 wakijeruhiwa.

Mripuko huo ulioharibu maelfu ya nyumba na biashara, ulitanguliwa na moto mkubwa katika ghala ya bandarini ambako mamia ya tani za kemikali ya Ammonium Nitrate ziliripuka.

Mwaka mmoja baadaye, uchunguzi uliofanyika bado haujatowa majibu ya nani aliamuru uagizaji wa kemikali hizo na kwa nini maafisa walipuuzia tahadhari za mara kwa mara za kuwepo na kitisho.

Ripoti ya kurasa 650

Kwenye ripoti hiyo yenye kurasa 650 iliyopewa kichwa cha habari "Walituua kutoka ndani", Human Rights Watch imechapisha orodha ya nyaraka na mawasiliano baina ya maafisa wa Lebanon juu ya kemikali ya Ammonium Nitrate iliyohifadhiwa kiholela kwa karibu miaka sita katika bandari.

"Hatua na kutojali kwa mamlaka za Lebanon kulitengeneza hatari ya maisha isiyo na sababu", imesema ripoti hiyo ikiongeza kuwa chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu, kitendo cha nchi kushindwa kuzuia kitisho cha wazi kwa maisha ni ukiukwaji wa haki ya binadamu.

Kwa nyongeza, HRW imedai kuwa ushahidi unaashiria vikali kuwa baadhi ya maafisa serikalini walifahamu uwezekano wa hatari itokanayo na uwepo wa kemikali hizo na wakapuuzia.

Ripoti hiyo imewataja maafisa waandamizi akiwemo rais Michel Aoun, waziri mkuu wa wakati huo Hassan Diab, mkuu wa zamani wa jeshi la Lebanon, maafisa wa ngazi ya juu wa usalama na mawaziri kadhaa miongoni mwa wengi ambao walitaarifiwa juu ya hatari iliyopo lakini walishindwa kuchukua hatua za kuulinda umma.

Maafisa wa Lebanon wamekiri kuwa walifahamu juu ya kemikali hizo na, ama wanadai kufuatilia suala hilo baada ya kufahamu au wanasema kuwa hawakufanya chochote kwasababu haikuwa ndani ya mamlaka yao.

Manusura wa mkasa huo na familia za wahanga wamekuwa wakitoa wito wa uchunguzi wa kimataifa, wakisema kuwa hawana imani na mfumo wa mahakama wa ndani.

Uharibifu uliojitokeza baada ya mripuko wa BeirutPicha: Reuters/A. Taher

Kemikali zilifikaje?

Mwaka 2013, Meli ya Rhosus iliyokuwa imebeba tani 2,750 za kemikali ya Ammonium Nitrate ilifika Lebanon ikitokea kwenye bandari ya Batumi kwenye bahari nyeusi. Ilikuwa ikielekea kwenye bandari ya Beira huko Msumbiji. Ilisimama katika bandari ya Beirut kwa ajili ya kusaka fedha za ziada kwa kubeba vipande kadhaa vya mashine kubwa. Lakini mzigo ulikuwa mkubwa na wafanyakazi wa meli hiyo waligoma kuubeba. Meli hiyo ilijipata katika mzozo na mamlaka za Lebanon ambazo zilidai meli ya Rhosus ilishindwa kulipa ada za bandari na hivyo haikuondoka bandarini hapo tena.

HRW inadai kuwa tangu wakati huo kumekuwa na maswali ikiwa ni kweli meli hiyo ilikusudiwa kufika Msumbiji au kama "Beirut ndio ilikuwa kituo cha kufikia".

Mwezi uliopita, jaji anayeongoza uchunguzi Tarek Bitar alisema anakusudia kuwashitaki wanasiasa waandamizi na wakuu wa zamani na wa sasa wa ulinzi na akaomba kibali cha kufungua mashitaka.

Kwa mujibu wa ripoti ya HRW, wale waliotajwa katika uchunguzi, akiwemo waziri mkuu anayeondoka, wabunge na magenerali wa juu, hadi sasa hawajafika katika ofisi ya mwendesha mashitaka mkuu na kuashiria kuwa pengine wana kinga kama sehemu ya bunge au wanahitaji kibali maalumu kutoka ofisi ya waziri mkuu au wizara ya mambo ya ndani.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW